Spurs yaiduwaza Man City, Chelsea yagawa dozi

Spurs yaiduwaza Man City, Chelsea yagawa dozi

Muktasari:

  • Ushindi ambao wameupata Tottenham Hotspur   wa mabao 2-0 dhidi ya Manchester City umewafanya kukwea hadi kileleni mwa msimo wa Ligi Kuu England wakiwa na pointi 20 huku wakiishusha Chelsea iliyokuwa ikiongoza kwa pointi 18.

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Tottenham Hotspur, Jose  Mourinho 'Special One'  ameonyesha umwamba   dhidi ya Pep Guardiola kwa kuliongoza chama lake likiwa nyumbani   kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Manchester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.

Son Heung-min  ndiye aliyeitanguliza  Spurs baada ya dakika tano tu za mchezo huo kuanza  akimalizia pasi  ya mwisho aliyotengenezewa na Tanguy Ndombele,  Manchester City ilipoteza uwezekano wa kuchomoa bao hilo dakika ya  27 baada ya  VAR kugundua kuwa  Gabriel Jesus aliugusa kwa mkono mpira kabla ya  Aymeric Laporte kufunga huku wwachezaji wa City wakionekana kutokubaliana na maamuzi hayo kiasio cha kumzonga mwamuzi Mike Dean wakiongozwa na nahodha wao Kelvin De Bruyne.

City  walikuwa na wastani mzuri wa umiliki mpira lakini hilo halikuwasaidia kwenye mchezo huo na wakajikuta wakiruhusu bao la pili walilofungwa na  Giovani lo Celso dakika ya 65 huku asissti ya bao hilo ikiwa  kutoka kwa   Harry Kane.

Wakati Pep Guardiola akitepeta kwa mara ya kwanza msimu huu mbele ya Mourinho hapo jana pia ilishuhudiwa Manchester United ikiibuka na ushindi  mwembamba wa bao 1-o dhidi ya West Brom lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Bruno Fernandes.

Michezo mingine ya mapema iliyochezwa Jumamosi, Chelsea iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 wakiwa ugenini dhidi ya Newcastle United huku Brighton wakiichakaza Aston Villa kwa mabao 2-1.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo, Jumapili  kwa michezo minne kuchezwa, Fulham itakuwa ikiikaribisha Everton, Sheffield Utd watacheza dhidi ya West Ham, Leeds itakuwa na kibarua mbele ya Arsenal huku  Liverpool wanaoandwama na majeruhi wakicheza dhidi ya  Leicester.

..................................................

Na Mwandishi wetu