Simbu aula Boston Marathon 2025

Muktasari:
- Katika orodha iliyotolewa na waandaaji wa mbio hizo juzi, jina la Simbu limejumuishwa huku la Gabriel Geay ambaye alishika nafasi ya pili katika mbio za Boston Marathon mwaka 2023 likiwa halipo.
MWANARIADHA nyota wa kimtaifa wa Tanzania, Alphonce Simbu ni miongoni mwa mastaa 10 ambao wamepewa mualiko wa kushiriki mbio za Boston Marathon 2025, huko Marekani zitakazoshirisha wanariadha waandamizi 23 kutoka nchi tofauti duniani.
Katika orodha iliyotolewa na waandaaji wa mbio hizo juzi, jina la Simbu limejumuishwa huku la Gabriel Geay ambaye alishika nafasi ya pili katika mbio za Boston Marathon mwaka 2023 likiwa halipo.
Tishio kubwa kwa Simbu katika mbio hizo ni Sisay Lemma wa Ethiopia ambaye anatetea medali yake ya dhahabu aliyoshinda katika mbio hizo mwaka jana akitumia muda wa saa 2:06:17, pia akitambia rekodi binafsi ya kutumia muda wa saa 2:01:48 katika mbio za Valencia Marathon 2023 ambayo ilimfanya ashike nafasi ya nne katika chati ya wanariadha waliotumia muda mfupi zaidi kumaliza mbio ndefu.
Ukiondoa Lemma, Simbu pia anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mshindi mara mbili wa mbio hizo, Evance Chebet ambaye mwaka jana alishika nafasi ya tatu pamoja na mshindi wa mbio za Chicago Marathon, John Korir.
Bingwa wa mbio za dunia 2024, Victor Kiplangat ni tishio jingine kwa Simbu kama ilivyo wa washindi namba mbili na namba tatu wa Berlin Marathon 2024, Cybrian Kotut na Haymanot Alew.
Mshindi wa mbio za Boston Marathon 2025 atapata kitita cha Dola 150,000, mshindi wa pili anapata Dola 75,000, wa tatu akipata Dola 40,000 na anayeshika nafasi ya nne anapata Dola 25,000.
Wakali watakaoshindani na Simbu kwenye Boston Marathon mwaka huu ni Sisay Lemma, John Korir, Evans Chebet, Cybrian Kotut, Haymanot Alew, Daniel Mateiko, Lelisa Desisa, Victor Kiplangat, Asefa Boki, Tebello Ramakongoana, Abel Kipchumba na Albert Korir.
Wengine ni Tsegay Weldlibanos, Patrick Tiernan, Conner Mantz, Clayton Young, Rory Linkletter, CJ Albertson, Amanuel Mesel, Erenjia Jia, Zach Panning na Colin Bennie.