Simba yakubali yaishe kwa Sven

Uongozi wa klabu ya Simba umethibitisha kuachana na kocha wake, Sven Vandenbroeck siku moja baada ya kuivusha timu hiyo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taarifa ya klabu hiyo imesema wameachana na kocha huyo kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Akiwa na Wekundu wa Msimbazi, Sven amepata mafanikio mbalimbali ikiwemo ubingwa wa Ligi Kuu, kombe la FA, ngao ya jamii.
"Kufuatia hatua hii kocha msaidizi Seleman Matola atakaimu nafasi iliyoachwa na Sven mpaka tutakapowatangazia atakayechukua nafasi hiyo hivi karibuni," imeeleza taarifa hiyo
Kikosi cha Simba kipo Zanzibar kujiandaa na mechi za Mapinduzi Cup.
Taarifa za ndani zinasema Sven ambaye ameondoka mchana wa leo kupitia Ethiopia, si kama alikuwa na matatizo dhidi ya uongozi wa Simba bali ni maamuzi yake binafsi.
Habari kutoka ndani ya Simba ambazo Mwanaspoti imezipata mchana wa leo, Sven alikutana na C.E.O wa Simba, Barbara Gonzalez na kumueleza uamuzi wake.
Baada ya vuta nikuvute kati ya Barbara na Sven walifikia uamuzi wa kocha huyo kuiacha Simba na kurudi kwao kwa madai ya kutaka kuwa karibu na familia yake.
Barbara alimsindikiza Sven hadi Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, kabla ya kuagana na muda mfupi kocha huyo kuanza safari.
Baada ya tukio hilo Barbara alifanya kikao cha kifupi na baadhi ya viongozi kujadili suluhisho ya jambo hilo na ambaye atakiongoza kikosi hiko.
Maamuzi ya kikao hiko kifupi yalitoka na maamuzi ya uongozi wa mabingwa hao watetezi wa Ligi kutafuta kocha mpya ambaye atakuja kuchukua mikoba ya Sven.
Wakati wakiendelea na mchakato huo kuna mawasiliano ya karibu na Sven ambaye wanajaribu kumshawishi ili kurudi katika majukumu yake.