Simba watua kimafia Kigoma kuwavaa Yanga

Thursday July 22 2021
kutua pic
By Ramadhan Elias

KIGOMA. BAADA ya asubuhi Yanga kuwasili kwenye uwanja wa ndege Kigoma na kuelekea moja kwa moja kwenye hoteli ya Mwitongo kupumzika, wapinzani wao Simba nao wametua jioni hii kimafia na kuelekea kwenye Hotel ya Lake Tanganyika.

Simba wametua uwanjani hapo saa 12:03 jioni na ndege ya Air Tanzania na kushuka ambapo moja kwa moja waliingia kwenye magari mawili aina ya Coasta yaliyokuwa eneo la ndani ya uwanja huo.

Sio kawaida kwa wanaoingia uwanjani hapo na ndege kupita mlango wa nyuma ya uwanja huo lakini Simba wamefanya umafia huo huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo Barbara Ngozalez akipita pekee kwenye eneo lililozoeleka.

Pili wakati Simba wanatua, hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kuingia ndani ya uwanja wa ndege kwani viongozi wa timu hiyo mkoni Kigoma waliweka masharti na ulinzi mkali eneo hilo.

Hata hivyo wachezaji hao na benchi la ufundi waliondoka uwanjani hapo mikono mitupu bila mabegi yao ambayo yalipakizwa kwenye troli na kupita lango kuu la uwanja huo kwaajili ya ukaguzi.

Bada ya hapo timu hiyo ilipokelewa na maelfu ya mashabiki waliokuwa wakiwasubiri kwa shauku kubwa nje ya uwanja huo wakicheza mziki na wengine wakishangili mwanzo mwisho.

Advertisement

Costa hizo za Simba zikiongozwa na gari la Polisi zilianza msafara wa kuelekea katika hoteli hiyo ambapo barabara zote za kuelekea hotelini zilijaa mashabiki wa timu hiyo wakiwemo waendesha pikipiki ‘Bodaboda’ na watembea kwa miguu.

Ujio huo wa Simba Kigoma ni kuelekea kwa mechi ya fainali ya kombe la Azam (ASFC) inayotarajiwa kupigwa Jumapili ya Julai 25, kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Advertisement