Mwenyekiti Simba atuliza upepo Msimbazi

Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amewataka mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kuwa watulivu.

Murtaza amesema katika kipindi hiki ambacho timu hiyo imekuwa ikipitia kwa uongozi wao na kuendelea kuweka akili zao katika mchezo muhimu wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga mchezo unaotarajiwa kupigwa Julai 25 katika uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma.

Kiongozi huyo alisema kuwa uongozi wa Simba upo makini na ulishatoa maelekezo ya kutatua mgogoro unaoendelea katika timu hiyo kati ya Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na Msemaji Haji Manara huku Mangungu akisema kuwa Simba ni timu inayojipambanua kuendeshwa kiweledi, hivyo wasimame katika misingi hiyo kwa kuwa wote wanaolumbana ni waajiriwa na mwajiri.

Aidha Murtaza alisema kuwa baada ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kumalizika timu hiyo itafanya tathimini ya mwenendo mzima wa timu hiyo na watendaji wake ila kwa sasa akiwataka kila mmoja  kuzingatia nidhamu, hekima na misingi ya ajira au nafasi yake katika timu huku akiwataka kuwa watulivu na kuendelea na mikakati ya michezo ijayo.  


IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI