Yanga yatua kibabe Kigoma

KIKOSI cha timu ya Yanga kimetua salama mkoani Kigoma ikiwa ni siku tatu zimesalia kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Simba mchezo unaotarajiwa kuchezwa Julai 25 katika uwanja wa Lake Tanganyika.

Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi wa soka nchini kutokana na uhasama mkubwa wa timu hizo lakini pia matokeo ya mwisho baina ya timu hizi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya pande hizo mbili yanachangia kuvuta hisia kubwa.

Wakati Yanga wakitua Kigoma wapinzani wao Simba wanatarajiwa kuondoka leo saa 9;50 alasiri huku timu hiyo ikipata mzuka zaidi kuelekea mchezo huo baada ya nyota wake Bernard Morrison kurejea nchini akitokea kwao Ghana alipokwenda kwa ajili ya mapumziko mafupi baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hii inakuwa ni mara ya nne kwa timu hizi kukutana msimu huu baada ya awali kukutana kwenye Ligi kuu Bara na kutoka sare kabla ya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo uliochezwa Julai tatu katika uwanja wa Benjamin Mkapa huku pia Simba akiwa na kumbukumbu ya kupoteza katika mchezo wa fainali dhidi ya Yanga kwenye kombe la Mapinduzi mwaka huu visiwani Zanzibar.

Hata hivyo Yanga inaenda katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa kwenye mechi ya mwisho ya Kombe hilo la Shirikisho la Azam (ASFC) wakati timu hizo zilipokutana mwaka jana kwenye hatua ya nusu fainali na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.  


IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI