Simba waitangulia Yanga

Simba imekuwa timu ya kwanza kuwasili uwanjani kwa ajili ya mechi yao ya fainali dhidi ya Yanga itakayoanza saa 2:15 usiku ambapo imeingia Uwanja wa Amaan saa 12:43 jioni.

Simba wanacheza mechi ya Fainali ya Kombe la Mapinduzi huku kocha wao Selemani Matola hajabadilisha kikosi chake kilichocheza mechi ya nusu fainali dhidi ya Namungo Fc huku Yanga wakiitoa Azam FC.

Kwa upande wa Yanga wamewasili uwanjani hapo saa 1:04 usiku na kocha Cedric Kaze amemuongeza Saido Ntibazonkiza kwenye kikosi chake cha kwanza kitakachoanza.

Yanga: Farouk Shikhalo, Kibwana Shomari, Adeyun Salehe, Said Makapu, Abdallah Shaibu, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Zawadi Mauya, Michael Sarpong, Said Ntibanzonkiza na Haruna Niyonzima.

Simba: Beno Kakolanya, David Kameta, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Joash Onyango, Tadeo Lwanga, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Francis Kahata na Miraji Athuman.


Hali ilivyokuwa Uwanjani

Milango yote ya uwanja huo ilifunguliwa saa 7 mchana ambapo mashabiki walianza kuingia taratibu lakini kuanzia saa 11 jioni ongezeko la mashabiki lilizidi huku jukwaa la mashabiki waliolipa kiingilio cha Sh 5,000 ndiyo likionekana kidogo lina mwanya tofauti na jukwaa kuu la Sh 15,000 na 10,000.

Mashabiki hao wameonekana kuwa na shauku kubwa ya kushuhudia mtanange huo ambapo kwa kisiwani hapa ni miaka mingi imepita timu hizo tangu zikutane ikiwa ni mwaka 2011 walipocheza fainalu na mashindano hayo.

Hata hivyo, nje ya uwanja kunaonekana kuwa na mashabiki wengi zaidi huku ikihofiwa kushindwa kuingia kushuhudia mpambano huo kwani uwanja una uwezo wa kuingiza mashabiki 12000 tu.