Simba waanza safari kurudi Dar na kombe lao

Mabingwa wapya wa Kombe la Mapinduzi Simba wameanza safari ya kurejea Dar es Salaam baada ya fainali za mashindano hayo zilizofanyika jana usiku Uwanja wa Amaan, Unguja.

Simba walitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Azam bao 1-0 lililofungwa na Meddie Kagere kwa mkwaju wa penalti baada ya Pape Sakho kufanyiwa faulo na kipa wa Azam Mathias Kigonya.

Simba wanarejea Dar ambapo kesho wataondoka kwenyr Mbeya kwa ajili ya mechi ya ligi kuu Bara dhidi ya Mbeya City itakayochezwa Januari 17 Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Simba iliifunga Azam ikiwa ni mara yao ya tatu kukutana kwenye fainali hizo ambapo mara mbili ilifungwa na matajiri hao wa ligi nchini Tanzania.

Mwenyewe wa Simba, Murtaza Mangungu amesema kuwa; "Tumemaliza hili na tumeanza mwaka vizuri tunaenda Mbeya kupambana ili kutetea ubingwa wetu wa ligi kuu.

"Mashindano yalikuwa magumu hata hii mechi ya mwisho ilikuwa ngumu sana hadi kupata ushindi ambao Azam walikuwa wakiusaka kwa hali na mali," amesema Mangungu