Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba waache ubinafsi kwenye hili

SIMBA Pict (1)
SIMBA Pict (1)

Muktasari:

  • Picha za marudio ya baadhi ya mechi huonyesha jinsi mshambuliaji gwiji wa Barcelona, Lionel Mersi alivyokuwa akidhibitiwa kwa nguvu na mchezo mchafu kila anapopata mpira katika mechi kati ya mahasimu hao ambazo hujulikana kama El Clasico. Mabeki kama Pepe walionekana kama wenye chuki binafsi na Messi.

KLABU za Barcelona na Real Madrid zina upinzani wa hali ya juu uwanjani na wakati fulani wachezaji huonekana kama wana chuki dhidi ya timu moja, kiasi kwamba baadhi ya mechi kati ya vigogo hao wa soka Hispania hutawaliwa na minyukano sehemu tofauti za uwanja.

Picha za marudio ya baadhi ya mechi huonyesha jinsi mshambuliaji gwiji wa Barcelona, Lionel Mersi alivyokuwa akidhibitiwa kwa nguvu na mchezo mchafu kila anapopata mpira katika mechi kati ya mahasimu hao ambazo hujulikana kama El Clasico. Mabeki kama Pepe walionekana kama wenye chuki binafsi na Messi.

Pia ukifuatilia kauli za wachezaji kama Gerard Pique dhidi ya Real Madrid utaona chuki ya wazi dhidi ya vigogo hao wa jijini Madrid, kiasi kwamba hata lingefanyika jambo gani, asingeweza kushawishika kujiunga na wapinzani hao.

Kitendo cha Luis Figo na Ronaldo de Lima kuchezea Real Madrid baadaye katika maisha yao baada ya kucheza Barcelona, kiliwapotezea hadhi yao ya ugwiji na hivyo hawapati heshima ambayo nyota wengine kama Messi wanaipata klabuni hapo.

Lakini nje ya uwanja, hasa katika masuala yanayohusu kupigania haki na uchumi, klabu hizo mbili ni marafiki na washirika wakubwa na huwa upande mmoja wakati wote.

Awali, klabu hizo ndio zilikuwa zikipokea mapato makubwa ya haki za televisheni kutokana na ukubwa wao, si katika soka la Hispania tu, bali duniani kote. Klabu nyingine za La Liga zilipoanza kudai malipo yanayolingana na viwango katika msimu, Barca na Real zilisimama pamoja hadi suala hilo lilipopatiwa ufumbuzi ambao uliondoa gawio lao kubwa kupita kiasi.

Wakati mpango wa kuanzisha Super League ya Ulaya, ambayo ingekuwa na mapato makubwa kwa klabu, Real Madrid na Barca zilisimama pamoja na klabu nyingine kubwa Ulaya kama Liverpool, Juventus na Arsenal kupigania mashindano hayo hadi mashabiki walipoingilia kati na vyama vya nchi kuzuia klabu zake.

Wakati Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) ilipowasilisha pendekezo kwa klabu kuuza asilimia 10 ya haki zao za kibiashara kwa kampuni ya CVC Capital Partners ya Marekani, Real Madrid, Barcelona, Atletico Madrid na klabu moja ya ligi daraja la pili, ndio pekee kati ya klabu 42 za ligi mbili za juu nchini Hispania, zilizokataa mpango huo uliowezesha kupatikana kwa Euro 2.1 bilioni mwaka 2021.

Mpango huo ulihusu kuuza asilimia 10 ya haki zao za kibiashara kwa miaka 50, jambo ambalo lilipingwa vikali na vigogo hao. Baadaye, Barcelona iliuza haki zake kwa kampuni nyingine.

Kwa hiyo, uwanjani Barca na Real ni wapinzani wakubwa lakini katika masuala ya maendeleo ya mchezo wenyewe, haki za kibishara na masuala mengine wanakuwa marafiki wakuu na hawategeani katika kuchukua hatua.

Wakati mwingine ni lazima masuala ya kimpira ya Tanzania yazungumzwe kwa mapana yake kwa kuangalia mifano mikubwa duniani. Sakata la mechi ya Simba na Yanga iliyoahirishwa kijanjajanja na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi na suluhisho la mgogoro huo linaonyesha ni kwa kiasi gani klabu hizo mbili haziwezi kusimama pamoja katika masuala muhimu ya kimpira.

Inawezekana kabisa sakata hilo likawa linaegemea upande mmoja kati ya pande hizo mbili, lakini suluhisho lake linatakiwa liwe la kujenga misingi mizuri ya uamuzi huko mbele badala ya kuliacha limalizike kimazoea na kujenga marejeo mabaya kwa uamuzi wa baadaye.

Shinikizo la Yanga kutaka Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ivunjwe, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo wajiuzulu linaweza kuwa limekwenda mbali sana kwa jinsi klabu nyingine zisivyolalamikia uamuzi mbovu au masuala mengine muhimu kwa maslahi ya klabu.

Lakini ukweli kwamba uamuzi wa kuahirisha mechi ulifanywa kwa kupapasa kanuni za kuhalalisha, hauwezi kuachwa eti kwa sababu tu, uliinufaisha Simba ambayo ilitishia kugomea mechi ya Machi 8. Simba inapaswa kuona udhaifu uliojitokeza katika kufanya uamuzi huo, ikijua kuwa mbinu hiyohiyo inaweza kutumiwa baadaye kuinufaisha Yanga badala ya kuonyesha kila wakati kuwa haina tatizo na haioni tatizo.

Ni wazi kwamba kwa kuwa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72) ilitangaza kuahirisha mechi kabla ya muda wa kuanza mchezo, ilifuta uwezekano wa Simba kuadhibiwa kama isingepeleka timu uwanjani (taarifa za uhakika zinasema Simba ilisharuhusu wachezaji wake waondoke kambini asubuhi siku ya mechi), lakini vipi iwapo uamuzi kama huo utafanywa siku ambayo itakuwa tayari kupeleka timu uwanjani na wapinzani wake wakagomea?

Kuzungumza kishabiki kwamba Simba iko tayari kupeleka timu uwanjani, ni kujaribu kupoozesha tatizo kubwa la uwajibikaji mbovu na tatizo la kuwepo kwa mianya ya kufanya uamuzi kiholela, jambo ambalo ni hatari kwa kila klabu.

Kitendo cha Simba kuponda shinikizo la Yanga kutaka watendaji wakuu wa TFF na TPLB wajiuzulu kwa madai kuwa ligi ina klabu 16 hivyo si sahihi kwa klabu moja kushinikiza kujiuzulu kwa viongozi hao, ni upofu wa kutoona ukubwa wa tatizo kwa mwingine.

Simba haikutakiwa hata kuzungumzia shinikizo hilo kwa kuwa haliihusu, hata kama kwa upande mmoja linahusisha dosari ambayo Simba inahusishwa. Itakuwaje siku nyingine mmoja wa watendaji hao atakapofanya kosa litakaloigharimu Simba? Watasema hawataki ajiuzulu kwa sababu kuna klabu 16?

Siku si nyingi Simba ilikuwa ikilalamikia uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuhusu kupanga Uwanja wa Amaan utumike kwa mechi ya marudiano ya fainali badala ya Uwanja wa Benjamin Mkapa. Kusingekuwa na hoja za msingi za kuhalalisha uamuzi huo, hadi leo Simba ingekuwa inalalamikia suala hilo na pengine ingeweza hata kuhusisha na matokeo. Lakini kwa kuwa kuna misingi mizuri ya kufanya uamuzi na mfumo mzuri wa kutoa taarifa, Simba ilikosa hoja zaidi.

Hoja ya Yanga kuwa muundo wa Bodi ya Ligi ubadilishwe na chombo hicho kiwe huru, ni kitu ambacho klabu zote zilitakiwa kupaza sauti, tena si wakati huu tu, bali kuanzia miaka zaidi ya kumi iliyopita.

Muundo wa Bodi ya Ligi hauna mfumo mzuri wa uwajibikaji na uwazi kwa kuwa mtu mmoja anaingia kwenye vikao vitatu tofauti vilivyotakiwa viwe vya kufuatilia uwajibikaji wa kila kimoja. Lakini kwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ndiye Mwenyekiti wa vyombo vingine, hakuwezi kuwa na uwajibikaji fanisi wala uwazi labda kuwe na ustaarabu wa hali ya juu kwa wahusika.

Muundo mzuri wa bodi utaihakikishia uhuru wake katika kufanya uamuzi. Uhuru wake pia utazihakikishia klabu ushiriki fanisi katika kufanya uamuzi. Taarifa ya Kasongo kuhusu mazungumzo na uongozi wa Yanga inadhihirisha kuwa Bodi haiwezi kufanya uamuzi wowote mgumu bila ya mamlaka za juu, ambazo zimejipachika jina la ‘sisi ndio wenye mpira’.

Ukosefu wa uhuru huu wa Bodi ya Ligi unaweza kuigharimu timu yoyote wakati wowote na hakuna haki ya kuwawajibisha watakaofanya makusudi kukosea.

Hakuna shaka kwamba baada ya kukosa ubingwa kwa miaka mitatu, viongozi wa Simba watatetea hata kile wanachoona si sahihi kwa kuwa kinaweza kuwasaidia kwa maslahi binafsi na si ya mpira, lakini hiyo ni kufikiria hadi mwisho wa mkono. Hoja za kuboresha muundo wa ligi haziwezi kupuuzwa wala kukejeliwa hata kidogo.

Bodi ya Ligi ilitakiwa iwe na muundo wa mashirika makubwa (corporate organisations) kwa kuwa mpira sasa unaendeshwa kibiashara zaidi na unahitaji viongozi na watendaji wenye maono, ujuzi na ufahamu wa uendeshaji biashara kuliko kupatikana katika kampeni za uchaguzi.

Katika biashara, kuheshimu sheria, kanuni, maadili na kuzingatia soko, ni vitu muhimu sana. Uamuzi usiofuata sheria, kanuni wala kuzingatia soko unaua biashara ya mpira wa miguu na hivyo ni lazima kuwe na viongozi kuanzia ngazi ya klabu ambao wana maono na si kuzingatia maslahi binafsi ya viongozi wa wakati huo tu.

Simba walitakiwa kuonyesha ukomavu huu katika sakata zima na si kuwa upande wa kudhihaki jitihada za wapinzani wao ambazo zinaweza kuwa msaada mkubwa kwao pale zitakapofanikisha kujenga chombo huru, chenye uwazi, kinachowajibika na kilicho imara katika kuendesha na kusimamia ligi.