Simba tupeni raha

Muktasari:

AFE beki au kipa, ndicho wanachotakiwa kukifanya Simba ili kujihakikishia safari ya kuendelea kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

AFE beki au kipa, ndicho wanachotakiwa kukifanya Simba ili kujihakikishia safari ya kuendelea kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba leo inashuka uwanjani ikiwa ugenini jijini Lusaka kucheza dhidi ya Red Arrows katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho huku wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo uliopigwa Novemba 28 katika Uwanja wa Mkapa.

Kocha wa timu hiyo, Pablo Franco atakuwa amejifunza kilichomkuta Didier Gomes, aliyeshinda ugenini mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy, lakini akageuziwa kibao nyumbani wakati wa mechi ya marudiano kwa kuchapwa mabao 3-1, Uwanja wa Mkapa.

Simba katika mchezo uliopita walionyesha kuhitaji matokeo ya haraka baada ya kucheza soka la kushambulia, lakini kikwazo kikubwa kilikuwa ni uwanja uliojaa maji kutokana na mvua.

Licha ya changamoto hiyo Simba walipambana kuhakikisha wanapata ushindi na walifanikiwa huku nyota ya mchezaji Benard Morrison ikiwa juu baada ya kuwasumbua vilivyo Red Arrows.

Kwenye mchezo huu Simba watakuwa na kibarua kingine cha kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwa wapinzani wao baada ya mwaka 2018 kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kufungwa 2-1 na Nkana na mchezo wa marudiano Simba waliichapa Nkana 3-1.


WAWADUWAZA ARROWS

Katika kuepuka janja janja ya Wazambia, Simba waliamua kujitegemea kila kitu baada ya kuwasili nchini humo lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha wanapata ushindi na kusonga mbele hatua inayofuata ya makundi

Mratibu wa Simba, Abbas Ally alisema wamejipanga nje na ndani ya uwanja huku wakiwasiliana na Shirikisho la Soka la Zambia (FAZ), tangu walipowasili nchini humo, wakikwepa kupokelewa na wenyeji wao Red Arrows.

“Wenzetu walijiandaa kutupokea tutakapowasili, lakini tuliwashangaza maana hatukuwapa taarifa za lini tunaenda bali tulikuwa tunawasiliana na shirikisho husika, jambo lililowashangaza ingawa yalikuwa ni malengo yetu ili kuepuka vitendo vyovyote viovu ambavyo wanaweza kuvifanya,” alisema.

Abbas alisema wamechukuwa tahadhali zote za Uviko-19 na timu nyingi za Afrika zimekuwa zikitumia kigezo hicho pindi zinapotafuta matokeo.

“Hatua zote muhimu tulizichukua ndio maana baadhi yetu tulifika muda mrefu hapa kabla ya timu kuwasili, hii inaonyesha ni kwa jinsi gani tumejipanga, tunachosubiria ni mchezo husika tu,” alisema Abbas.

Timu hizo zinakutana katika mchezo wa pili wa marudiano utakaopigwa Uwanja wa Nkoloma mjini Lusaka.


ALICHOSEMA KAGERE

Straika wa timu hiyo, Meddie Kagere alisema wamejiandaa kupambana hadi tone la mwisho kuhakikisha wanatinga hatua inayofuata kwenye michuano hiyo.

“Hii ni nafasi ya dhahabu kwetu, lazima tuipambania kwa ari na nguvu zetu zote, kwani Simba ndio timu pekee iliyosalia kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano hii, hivyo lazima tujitoe hadi tone la mwisho,” alisema.

Naye kocha wa timu hiyo, Pablo hakuwa nyuma kuzungumzia mechi hiyo, ni ngumu ila wameunganisha nguvu yao, kuhakikisha wanarejea Tanzania kwa kishindo.

“Najua tunacheza ugenini, ila tunakwenda kupambania nafasi adimu kuhakikisha tunaendelea kuwepo kwenye michuano ya Caf,” alisema.

Imeandikwa na Olipa Assa, Thomas Ng'itu na Daud Elibahati