Simba noma, yaingia anga za vigogo Afrika

SIMBA wajanja sana kwani baada ya juzi usiku kumalizana na Dodoma Jiji, fasta imegeuza kurudi jijini Dar es Salaam ili kuajindaa na mechi ya Kombe la ASFC dhidi ya Coastal Union, huku ikiiwahi mapema AC Horoya ya Guinea watakayovaana nayo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba na Coastal zitakutana Januari 28 Kwa Mkapa kabla ya kuanza vita ya michuano ya CAF katika Kundi C la Ligi ya Mabingwa na katika kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, mabosi wa klabu hiyo wameamua kutanguliza watu Guinea, wakichakarika pia kupata vibali vya kwenda huko.

Wakati wachezaji wakipewa mapumziko hadi kesho ili kuanza maandalizi ya mechi ya Kombe la ASFC, klabu hiyo imepanga kutuma watu wawili Guinea akiwamo mratibu Abbas Ali Suleiman kwenda kuweka mambo sawa kabla ya timu kusafiri kwa mchezo wa kwanza wa ugenini dhidi ya Horoya.

Mipango ya viongozi ni kuona wanashinda mechi hiyo na ikishindikana kabisa iambulie japo sare ili kujiweka pazuri katika kundi hilo lenye timu za Vipers ya Uganda na Raja Casablanca ya Morocco.

Abbas na kiongozi mwingine watakwenda kutafuta hoteli nzuri watakayofikia msafara mzima wa timu hiyo, kuweka mipango ya magari watakayotumia, uwanja wa kufanyia mazoezi mepesi siku mbili kabla ya mchezo pamoja na ishu za misosi na vinywaji mbali na mambo mengine ya msingi.

Aidha, huku nyumbani, viongozi waliosalia walianza mapema kazi ya kuhakikisha wachezaji wote wakiwamo walio majeruhi, benchi la ufundi pamoja na baadhi ya viongozi wanapeleka hati zao za kusafiria (pasipoti) kwenye Ubalozi wa Guinea uliopo Upanga, Dar es Salaam kwa ajili ya kuomba visa.

Pasipoti hizo zinaelezwa zimepelekwa mapema ubalozini na hadi sasa zoezi la kupata visa lipo hatua ya mwishoni kwani ili kuzipata huchukua si chini ya wiki mbili na wamefanya hivyo kwa lengo la kukwepa usumbufu wa kulifanya zoezi hilo zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kusafiri.

Kwa mujibu wa ratiba ya mechi za makundi, Simba itacheza mechi ya kwanza Februari 10 dhidi ya AC Horoya na klabu hiyo imepanga kuondoka kati ya Februari 7-9.