Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba kuupiga mwingi na pointi juu

Muktasari:

SIMBA wanasema kama unataka burudani ya soka, we kicheki kikosi chao kikishuka uwanjani jioni ya leo, kwani wataupiga mwingi na kufunga mabao ya kutosha ili kubeba alama tatu za kwanza katika mechi zao tatu za Ligi Kuu Bara Kanda ya Ziwa.

SIMBA wanasema kama unataka burudani ya soka, we kicheki kikosi chao kikishuka uwanjani jioni ya leo, kwani wataupiga mwingi na kufunga mabao ya kutosha ili kubeba alama tatu za kwanza katika mechi zao tatu za Ligi Kuu Bara Kanda ya Ziwa.

Watetezi hao wanavaana na Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga, huku nyota wa timu hiyo wakisisitiza hawana kingine walichokifuata mkoani humo ila kuwapa burudani mashabiki wao na kunyakua alama tatu za kutetea taji lao kwa mara ya nne mfululizo.

Mwendelezo wa matokeo mabaya ya wenyeji wao na ubora wa kikosi cha Msimbazi ni mambo mawili yanayoipa jeuri Simba kuibuka na ushindi dhidi ya Mwadui leo ikiwa ugenini, japo wanakumbukumbu ya mechi za nyuma baina yao uwanjani hapo na kushuka kwa tahadhari kubwa.

Ikiwa imecheza mechi 14 mfululizo za Ligi Kuu bila kupoteza, Simba itaingia uwanjani ikiwa na furaha ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliopita, huku wenyeji wao wakipambana kuepukana na jinamizi la kushuka daraja, wakicheza mechi saba bila kushinda.

Mwadui imecheza mechi hizo ikipoteza sita na kutoka sare moja tu, kitu kinachotoa picha mbaya kwao wanapovaana na Simba iliyo moto msimu huu chini ya Kocha Didier Gomes.

Simba imekuwa haina historia nzuri na mechi za Kanda ya Ziwa na mara nyingi imeshindwa kukusanya pointi zote kutoka timu zilizopo katika kanda hiyo.

Pia Simba ina kumbukumbu isiyofurahisha mbele ya Mwadui ambayo msimu uliopita ilivunja rekodi yao ya kutopoteza mechi saba mfululizo pale ilipowafunga kwa bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza baina yao.

Katika mchezo huo uliochezwa Oktoba 30, 2019. bao pekee la Mwadui FC lilifungwa na Gerard Mdamu aliyepo Polisi Tanzania kwa sasa.

Kijumla Simba imekuwa ikikutana na changamoto mbele ya Mwadui pindi zinapokabiliana huko Shinyanga na uthibitisho wa hilo ni mechi tano za Ligi Kuu zilizowakutanisha kwenye Uwanja wa Kambarage na Simba imeibuka na ushindi mara mbili, ikifungwa moja na mechi mbili wakitoka sare.

Ushindi katika mechi ya leo utaifanya Simba ifikishe jumla ya pointi 52 na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri katika mbio za ubingwa ukizingatia watabakia na mechi tatu mkononi ambazo wakishinda watafanya pengo la pointi baina yao na Yanga na Azam kuwa kubwa.

Kwa upande wa Mwadui wanaoshika mkia katika msimamo wa ligi, ushindi utawafanya wafikishe pointi 21 na hivyo kuwafanya angalau wawe na matumaini ya kubaki Ligi Kuu au kucheza mechi za mchujo, vinginevyo watajiweka katika nafasi finyu ya kubaki Ligi Kuu.

Wakati Simba wakiingia katika mechi ya leo huku nguvu yao kubwa ikiwa imeonekana kukamilika kila idara, ni tofauti na Mwadui ambayo safu yake ya ulinzi imekuwa ikiwaangusha.

Simba imefunga jumla ya mabao 51 na kuruhusu mabao tisa tu wakati Mwadui licha ya washambuliaji wake kujitutumua na kufunga mabao 18, safu yake ya ulinzi imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 46.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema pamoja na Mwadui kuwa na mwendelezo wa kufanya vibaya, wanaingia katika mechi hiyo wakiwa na tahadhari kubwa.

“Naamini utakuwa mchezo mgumu kwa sababu Mwadui FC hawako katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi na wanahitaji kujinasua lakini lengo letu kama timu ni kupata ushindi dhidi yao na mechi nyingine mbili tutakazocheza dhidi ya Kagera Sugar na Gwambina ili tuweze kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi.

Ratiba imetubana sana lakini naamini tunaweza kufanya vizuri katika michezo yetu na haipaswi kuwa kisingizio,” alisema Gomez.

Naye Kocha wa Mwadui, Salhina Mjengwa alisema wamejipanga vyema kuikabili Simba katika mechi ya leo.

“Maandalizi yetu yako vizuri, tunafahamu tunacheza na timu nzuri, hivyo tumejipanga vyema na malengo yetu ni kupata ushindi katika mechi hiyo,” alisema Mjengwa.

Katika Uwanja wa Ushirika Moshi, Polisi Tanzania itaikaribisha Tanzania Prisons mchana kabla ya saa 10 jioni, Simba na Mwadui zitakapomalizana Shinyanga, nazo Dodoma Jiji na Namungo zitakuwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kupepetana katika mfululizo wa ligi hiyo.