Simba, Kagera ni shoo shoo

Saturday May 01 2021
simba kagera 2 pic
By Charles Abel

HESABU nzuri dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa leo saa 1.00 usiku katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam ndizo zitakazoiweka Simba katika uwezekano mkubwa wa kurudia mafanikio iliyoyapata msimu uliopita au zaidi.

Msimu uliopia, Simba ilitwaa mataji matatu ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho (ASFC) na tayari msimu huu imeshatwaa taji la Ngao ya Jamii baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Namungo katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Agosti 30, 2020.

Simba ipo katika nafasi nzuri ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu ikiongoza msimamo ikiwa na pointi 61, nne mbele ya Yanga walio nafasi ya pili na pointi 57 wakati huohuo, Simba wakiwa na mechi mbili zaidi za viporo ambazo wakishinda watakuwa mbele kwa utofauti wa pointi 10.

Kadhalika Simba inafanya vyema katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo sasa wapo katika hatua ya robo fainali.

Pamoja na hayo, leo licha ya kiu ya ushindi waliyonayo ambao itawafanya watinge katika hatua ya robo fainali, wanapaswa kuingia kwa hesabu na tahadhari kubwa ili waweze kuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa mataji mawili makubwa ya soka nchini.

Hilo linachagizwa na ushindani mkubwa ambao Simba imekuwa ikikutana nao dhidi ya Kagera Sugar pindi wakutanapo ambapo mara kadhaa imejikuta ikipoteza mchezo ama ikicheza ugenini huko Kagera au hapa Dar es Salaam.

Advertisement

Ingawa imeibuka na ushindi katika mechi zote mbili za Ligi Kuu zilizopita walizokutana msimu huu, bado Simba ina kumbukumbu ya kichapo cha bao 1-0 ilichokipata nyumbani kutoka kwa Kagera, msimu wa 2018/2019 lakini pia Simba haohao walitibuliwa sherehe zao za kukabidhiwa Kombe la Ligi Kuu msimu wa 2017/2018 walipofungwa kwa bao 1-0 na Kagera mbele ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba pia ina kumbukumbu ya kutolewa mara tatu katika hatua za mwanzoni dhidi ya timu ambazo hazikuwa zikipewa nafasi kubwa ya kufanya hivyo ambapo msimu wa kwanza wa mashindano hayo ilitupwa nje na Coastal Union katika hatua ya robo fainali baada ya kufungwa kwa mabao 2-1, msimu wa 2017/2018 ikafungwa na Green Warriors kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika hatua ya 16 bora na msimu wa 2018/2019 ikatolewa na Mashujaa ya Kigoma katika hatua kama hiyo baada ya kufungwa mabao 3-2 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Huku Simba ikipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi, benchi lake la ufundi litakuwa mtegoni katika upangaji wa kikosi kwani pamoja na mechi kama hiyo kuhitajika kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao huwa hawapangwi mara kwa mara bado wanatakiwa kupanga kikosi imara kitakachoweza kuwakabili Kagera ambao wanasifika kwa kucheza soka la pasi na la kushambulia.

Wakati Kagera wakiingia katika mchezo wa leo wakiwa na pigo la kumkosa kocha wao mkuu, Francis Baraza ambaye amerudi kwao Kenya kuhudhuria mazishi ya mama yake mzazi, Simba wao watakuwa wako vizuri kisaikolojia hasa baada ya kufanikiwa kuwaongezea mikataba nyota wake wanne akiwamo John Bocco, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe.

Meneja wa Kagera, Paul Ngalyoma alisema wamedhamiria kuifunga Simba.

Advertisement