Simba hawashikiki, yaichapa Al Ahly

Tuesday February 23 2021
full pic
By Ramadhan Elias

Dar es Salaam. Mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Al Ahly imemalizika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wenyeji Simba wakiibuka na ushindi wa bao 1-0.


Bao la Simba lilifungwa kipindi cha kwanza na nyota wao machachari Luis Miquissone katika dakika ya 30 kwa shuti kali baada ya kuwahadaa mabeki wa Al Ahly na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika wakiongoza.

full pic 2


Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko kwa kumtoa Hassan Dilunga na nafasi yake kuchukuliwa na Rally Bwalya ambaye aliingia kucheza nafasi ya kiungo na kuonyesha utulivu katika eneo hilo.


Pia katika kipindi cha pili timu zote mbili ziliendelea na mchezo wa kucheza kwa tahadhari na kushambulia kwa kusitukiza huku kwa Simba ingizo la Bwalya likionekana kuwa na changamoto kwa Ahly.

full pic 1
Advertisement


Winga wa Simba Luis Miqquissone alionekana kuwapa wakati mgumu walinzi wa Ahly kila alipokuwa na mpira jambo lililowafanya kumchezea madhambi mara kwa mara hususani kipindi cha pili.


Simba kwenye kipindi cha pili walionekana kucheza bila presha kubwa, huku umakini ukiongezeka katika ukabaji ambapo safu ya ulinzi iliyoongozwa na Pascal Wawa na Joash Onyango ilionekana kuwa na maelewano thabiti.

full pic 3

Katika dkika ya 72 kocha wa Simba, Gomes Da Rosa alimtoa kiungo Taddeo Lwanga aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji mkongwe na kiraka katika kikosi hicho, Erasto nyoni.


Beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein alionekana kukumbwa na changamoto ya mbinu za Ahly kutaka kupitia upande wake, lakini alijitahidi kuonyesha umahiri kukabiliana na mashambulizi ya wapinzani wao.

Al Ahly ambao ni mabingwa mara tisa wa mashindano hayo pia walifanya mabadiliko ya jumla ya wachezaji watano ambayo kwenye mechi ya leo hayakuwaepusha na kichapo hicho ugenini cha bao 1-0.


Zikiwa zimebaki dakika tano katika mechi hiyo kumalizika Simba walifanya mabadiliko mawili kwa kuwatoa Chris Mugalu na Luis Miquissone na nafasi zao zilichukuliwa na Meddie Kagere na Fransic Kahata. Pia dakika ya 90 walimtoa Clatous Chama na nafasi yake kuchukuliwa na Kennedy Juma mabadiliko ambayo yalilenga kulinda bao lao.

Kwa ushindi huo Simba inapanda kileleni mwa kundi A wakiwa na alama 6, AS Vita (3), Al Ahly (3) na Al Merrikh (0).

Advertisement