Simba fainali Ligi ya Mabingwa Afrika ileeeee!

Muktasari:

SIMBA washindwe wenyewe tu sasa. Hii ni baada ya jana kufanyika droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayowakutanisha na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

SIMBA washindwe wenyewe tu sasa. Hii ni baada ya jana kufanyika droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayowakutanisha na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Takwimu na rekodi za uzoefu wa Kaizer Chiefs katika michuano hiyo zinawapa nguvu Simba na kuwaweka katika nafasi nzuri kisaikolojia kupata matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wao baada ya droo iliyofanyika jana alasiri jijini Cairo, Misri.

Simba imetinga robo fainali ikiwa na takwimu bora kitimu na hata kwa mchezaji mmojammoja kulinganisha na Kaizer Chiefs waliyoizidi kwa vipengele vingi kitakwimu.

Kaizer Chiefs imeonekana kuwa dhaifu katika safu ya ushambuliaji na hata ile ya ulinzi katika michuano hiyo tofauti na ilivyo kwa Simba, na ikiwa itashindwa kujirekebisha kazi inaweza kuwa nyepesi kwa wawakilishi hao wa Tanzania.

Katika mechi sita za hatua ya makundi, Kaizer Chiefs wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara sita ikiwa ni wastani wa bao moja katika kila mchezo na pia wamekuwa na udhaifu katika kushambulia kwani wamefunga mabao matano tu.

Hiyo ni tofauti na Simba ambayo katika mechi sita za hatua ya makundi imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu, huku ikifunga jumla ya mabao tisa.

Wawakilishi hao wa Afrika Kusini wamekuwa hawafungi idadi kubwa ya mabao wanapokuwa nyumbani kwani katika mechi tatu wamepachika mabao mawili tu na hilo linaweza kuwa na manufaa kwa Simba

Kwa ujumla, Kaizer Chiefs inayonolewa na Gavin Hunt imefunga mabao saba katika mashindano hayo msimu huu na kati ya hayo, kinara aliyefunga idadi kubwa ni beki Eric Mathoho ambaye amepachika mawili. Hiyo ni tofauti na Simba ambayo katika mechi zote za mashindano hayo msimu huu imefunga mabao 14, ambapo Clatous Chama ni kinara akifunga manne akifuatiwa na Luis Miquissone aliyefunga matatu, huku Chris Mugalu akipachika mawili.

Kaizer Chiefs wanaachwa mbali na Simba katika kipengele cha uzoefu kwani hii ni mara ya kwanza kutinga robo fainali na hata hatua ya makundi tangu mfumo wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ulipobadilishwa tofauti na Simba ambao hii ni mara ya pili kutinga hatua ya robo fainali huku wakiwa wametinga makundi mara tatu.

Simba itaanzia ugenini kwenye mechi itakayopigwa kati ya Mei 14 na 15 kabla ya kurudiana jijini Dar es Salaam Mei 21-22 ili kuamua hatima ya kufuzu nusu fainali.

Kama Simba itavuka salama itafikia rekodi ya 1974 ilipocheza na Mehalla Al Kubra ya Misri wakati michuano ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika.

Hata hivyo, nusu fainali Simba au Kaizer Chiefs inaweza kuvaana na kati ya Wydad Casablanca ya Morocco au MC Alger ya Algeria.

Baadhi ya mashabiki wa Simba wamechafua katika mitandao ya kijamii wakiamini timu yao ina nafasi kubwa ya kufika hata fainali kama itamalizana na Kaizer Chiefs kisha kukutana na Wydad anakocheza winga wa zamani wa Yanga, Saimon Msuva au Waalgeria ambao hawana maajabu makubwa Afrika.


WA KUCHUNGWA

Pamoja na Simba kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwatupa nje Kaizer Chiefs inapaswa kuwachunga nyota kadhaa wa timu hiyo ambao licha ya ubora wao, thamani waliyonayo sokoni imewafanya wawe wanatazamwa kwa jicho la karibu na timu mbalimbali pindi zikutanapo na timu hiyo ya Sauzi.

Kwa mujibu wa mtandao wa transfermarkt, mchezaji mwenye thamani kubwa sokoni wa Kaizer Chiefs kwa sasa ni mshambuliaji wa Zimbabwe, Khama Builliat ambaye pia anaweza kucheza kama winga au kiungo mshambuliaji mwenye thamani ya Euro 1.5 milioni (takriban Sh4.2 bilioni) akifuatiwa na kipa ambaye ni nahodha Itumeleng Khune mwenye thamani ya Euro 775,000 (takriban Sh2.3 bilioni).

Ukiondoa hao, wachezaji wengine wenye thamani kubwa na ambao wamekuwa tegemeo la Kaizer Chiefs ni Daniel Cardoso (Sh2.1 bilioni), Leonardo Castro (Sh1.8 bilioni), Eric Mathoho na Daniel Akpey ambao kila mmoja ana thamani ya Sh1.7 bilioni na Samir Nurkovic mwenye thamani ya Sh1.5 bilioni.


MSIKIE GOMES

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes alisema jana kuwa, kupangwa na Kaizer Chiefs ni faraja kwao, huku akikiri ni mara yao ya kwanza kukutana kwenye michuano hiyo, lakini kwa sasa anaweka akili yake kwenye mchezo wa leo dhidi ya Kagera Sugar katika michuano ya Kombe la ASFC.

“Tunataka kufika mbali kwenye mashindano haya na tupo tayari kucheza vizuri dhidi ya Kaizer Chiefs kwenye michezo yote.

“Haitakuwa rahisi, lakini nina uhakika huu msimu Simba inaweza kwenda mbali zaidi, ila mikakati juu yao kwa lengo la kuona tunafanya vizuri tutaanza baada ya kumalizana na mechi ngumu zilizopo mbele yetu. Tuna mchezo na Kagera kesho (leo) na baadaye dhidi ya Yanga.

“Tukimaliza mechi hizo ndipo tutajipanga zaidi kwa hatua hiyo ya robo fainali na hasa kuhakikisha tunafanya vizuri ugenini kabla ya kuja kumalizia mechi ya marudiano, ili kuwania kutinga nusu fainali,” alisema Gomes aliyeiandikia rekodi Simba ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kumaliza kama kinara wa kundi la michuano ya Afrika.

Simba iliongoza Kundi A ikiwa na pointi 13 mbele ya Al Ahly ambao ni watetezi wa michuano hiyo.


WADAU HAWA HAPA

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Mulamu Nghambi alisema mchezo huo utakuwa mgumu na wenye ushindani kwa kuwa kila timu iliyofikia hatua hiyo ni bora.

Alisema wao kama Simba wamejipanga kukutana na timu yoyote huko mbeleni wakiamini uwezo na nia ya dhati wanayo na kila mechi kwao ni fainali.

“Tumepokea vyema droo hii, kucheza na Kaizer kwa mechi zote zitakuwa ngumu, ila ni kwamba safari hii tuna jambo letu, hivyo haijalishi umepangiwa na timu gani,” alisema Mulamu.

“Tutahakikisha tunapambana tuvunje historia ya robo fainali ya mwaka juzi ili tufike nusu fainali na hatimaye fainali, uwezo tunao na tunaheshimu kila timu tunayokutana nayo.”

Naye mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema ratiba ipo poa kwa Simba hasa kuanzia ugenini, licha ya Kaizer Chiefs kuwa ni timu nzuri, ila uzoefu utawabeba Wekundu wa Msimbazi.

“Mchezo huo sina shaka na Simba kabisa, ni mechi nzuri hasa ikizingatia wanaanzia ugenini wanamalizia nyumbani, na uwezo, uzoefu walioupata nyuma utawasaidia sana,” alisema Mogella, huku kipa Ivo Mapunda, nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars akisema: “Njia mojawapo ya wao kwenda hatua inayofuata, kiwango cha Simba ni cha kimataifa zaidi, Simba ni klabu kubwa Afrika ina wachezaji wazuri na ni bora kila idara, cha msingi game plan (mpango wa mchezo) ndio wa kuangalia mapama.”