Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ouma hesabu kali taji la Shirikisho

OUMA Pict

Muktasari:

  • Mechi hiyo ya fainali inatarajiwa kupigwa Jumapili ya Juni 29 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja visiwani Zanzibar, Singida ikisaka taji la kwanza la michuano hiyo, huku Yanga ikitaka kutetea kwa msimu wa nne mfululizo.

LICHA ya kuwa na mechi ya kufungia msimu inayopigwa kesho dhidi ya Tanzania Prisons, benchi la ufundi la Singida Black Stars limesema litawekeza nguvu na akili katika pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya watetezi, Yanga ili kufunga msimu kwa heshima.

Mechi hiyo ya fainali inatarajiwa kupigwa Jumapili ya Juni 29 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja visiwani Zanzibar, Singida ikisaka taji la kwanza la michuano hiyo, huku Yanga ikitaka kutetea kwa msimu wa nne mfululizo.

Kocha wa timu hiyo, David Ouma alisema matokeo ya mechi za Jumatano ya wiki hii kwa Singuida kushinda mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji, kisha Azam kuwanyoosha Tabora United kwa mabao 5-0 imeshatoa picha ya nafasi kwa timu hiyo kumaliza ya nne.

Kutokana na hali hiyo kwa sasa hata mechi ya kesho dhidi ya Tanzania Prisons ni kukamilisha ratiba kwa heshima, lakini nguvu kubwa inaelekezwa katika mechi ya fainali ya FA ili wabebe taji kwa mara ya kwanza, kwani kwa Ligi Kuu ni kama wameshamaliza kazi mapema.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema wanachohitaji ni kumaliza vizuri pambano la mwisho la Ligi Kuu dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida, akiahidi kutakuwa na mabadiliko kadhaa ya wachezaji.

“Tutajaribu kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji kwa sababu tunaangalia uwezekano wa kuwalinda wasipate changamoto zozote, kutokana na umuhimu mkubwa wa mechi yetu ya fainali ya Kombe la Shirikisho la FA, dhidi ya Yanga,” alisema Ouma.

Kocha huyo Mkenya, alisema licha ya kuiwazia Yanga ila atahakikisha pia anatumia mechi na Prisons kwa ajili ya kumaliza vizuri msimu huu, kwa sababu kitendo cha kumalizia nyumbani ni heshima kubwa hasa kwa mashabiki waliopo mjini Singida.

“Mechi yetu ya Yanga itachezwa Juni 29, badala ya Juni 28 kama ilivyokuwa imepangwa awali hivyo, itatupa nafasi nzuri ya kuweka mikakati vizuri, tukidhamiria kuhitaji ubingwa wa michuano hiyo licha ya ubora pia wa wapinzani wetu,” alisema Ouma.

Ouma aliiongoza Singida tangu Februari 4, 2025, baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miloud Hamdi aliyetambulishwa Desemba 30, 2024, kuondoka kikosini na kujiunga na watetezi wa Ligi Kuu, Yanga anayoendelea kuifundisha sasa.

Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa akiwa na leseni A ya UEFA, aliondoka Singida bila ya kuiongoza katika mechi yoyote, ambapo alijiunga nayo ili kuchukua nafasi ya, Mbelgiji Patrick Aussems aliyeondoka rasmi Novemba 29, 2024.

Tangu Ouma akabidhiwe kikosi hicho kinachoshika nafasi ya nne na pointi 56, ameiongoza timu hiyo katika mechi 13 za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo ameshinda saba, akitoa sare mbili na kupoteza nne, huku akifunga mabao 20 na kuruhusu 12.

Ouma pia ameiwezesha Singida kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuamaliza nafasi ya nne nyuma ya Azam FC yenye pointi 60 ambazo haziwezi kufikiwa na Wauza Alizeti hao, hii ikiwa ni mara ya pili mfululizo, kwani msimu uliopita aliipeleka Coastal Union iliyotolewa raundi ya kwanza na Bravo do Marquis ya Angola kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0.