Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siasa, wafadhili vimeua soka Zanzibar- 1

Muktasari:

Ukipita maeneo mbalimbali visiwani humo hasa Unguja nyakati za jioni utaona makundi ya vijana wa umri mdogo wakicheza soka kwenye viwanja tofauti.

SOKA la Zanzibar limekuwa likizama siku hadi siku, mafanikio kama yale ya Malindi kucheza nusu fainali ya Kombe la CAF na Zanzibar Heroes kutwaa taji la Chalenji mwaka 1995 hayatoi dalili zozote za kujirudia. Fuatilia mfululizo wa makala haya ili ujue kwa undani nini hasa tatizo. Endelea…

Ukiachana na utalii, sifa nyingine kati ya nyingi katika Visiwa vya Zanzibar ni kuwa mstari wa mbele kuzalisha wachezaji wazuri wanaoweza kuonyesha vipaji vyao wakiwa katika umri mdogo.

Ukipita maeneo mbalimbali visiwani humo hasa Unguja nyakati za jioni utaona makundi ya vijana wa umri mdogo wakicheza soka kwenye viwanja tofauti.

Hali hiyo inaashiria kwamba visiwa hivyo vina watu wenye mapenzi na mchezo huo au vijana wengi wenye vipaji na ambao hawafundishwi soka ukubwani.

Pamoja na hayo yote lakini upo ukweli kwamba thamani na hadhi ya soka la Zanzibar imekuwa ikiporomoka siku hadi siku kiasi cha baadhi ya watu kufikia hatua ya kusema kwamba soka linakufa Zanzibar.

Hao ni wale ambao wanakumbuka enzi za soka la ushindani Zanzibar, miaka hiyo kulikuwa na timu maarufu zilizotoa ushindani wa ndani na wakati mwingine hata nje ya visiwa hivyo.

Ni enzi ambazo kulikuwa na timu kongwe na tishio kama Malindi, Small Simba, Kikwajuni, Shangani pamoja na timu ya Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) ambayo inaonekana kama ndiyo timu pekee iliyobakia pale unapozikumbuka timu za enzi hizo.

Ligi hiyo haikutawaliwa na timu za majeshi, mbali na Polisi Zanzibar na KMKM, timu nyingine nyingi imara zilikuwa timu za uraiani tofauti na sasa ambapo Ligi Kuu Zanzibar yenye timu 12, kati ya hizo saba ni za majeshi.

Ukikumbuka enzi hizo Zanzibar ikiwa gumzo katika soka, timu za Small Simba, Malindi, Kikwajuni, Shangani na KMKM zilichangia kuipandisha chati Ligi Kuu Zanzibar wakati huo ikijulikana kwa jina la Ligi Daraja la Kwanza.

Ushindani mkubwa uliokuwepo baina ya timu hizo na kuleta hamasa kwa mashabiki ambao walijikuta wanapenda kuangalia na kusaidia soka lakini sasa ni kinyume, timu hizo hazina nguvu na nyingine zimekufa kabisa.

Moja ya timu zilizokufa kabisa ni Mlandege, timu iliyokuwa na upinzani mkubwa visiwani humo hasa ilipokutana na Malindi, Small Simba, Kikwajuni na hata Shangani.

Upinzani huo ulitokana na ufadhili wa wakati huo kutoka kwa wafanyabiashara maarufu, Malindi ilifadhiliwa na Noushad Mohammed, Kikwajuni alikuwa chini  ya Ibrahim Raza wakati Shangani ilifadhiliwa na Mohammed Raza ambao wote kwa sasa hawajishughulishi na timu hizo.

Hata hivyo, Malindi ndiyo timu kongwe kuliko zote iliyozaliwa kabla ya mwaka 1940 ikiwa timu ya mtaani na mwaka huohuo ilipata jengo lake lililopo Mtaa wa Malindi, jengo ambalo lilinunuliwa na mfadhili wao na kuwa mali ya klabu hadi sasa.

Hata hivyo, mfadhili wa timu hiyo baadaye aliamua kujitoa kutokana na mambo ya kisiasa, lakini kazi aliyoifanya ilitosha kuwavuta watu wengi kujiingiza kwenye soka.

Malindi ndiyo klabu pekee inayoweza kuendesha shughuli zake kupitia rasilimali zake zilizoachwa na mfadhili wao huyo huku klabu kama Small Simba jengo lake likiwa limepangishwa watu wanaoishi humo na baadhi ya vyumba wamepewa wazee waanzilishi wa klabu hiyo.

Kwa upande wa timu ya Kikwajuni, wao jengo lao lipo tu na halifanyi shughuli yoyote. Mlandege wao hawana jengo na hawaeleweki kwa sasa wapo wapi.

Timu hizo kongwe baadhi yao hazipo kwenye Ligi Kuu Zanzibar kama Small Simba na Kikwajuni lakini Malindi na KMKM ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo bado zinadunda.

Malindi haifanyi vizuri kwenye ligi kila msimu, ipo kama haipo, mara zote inajitahidi kujinusuru na janga la kushuka daraja tu hali ambayo ni tofauti na KMKM, timu ya jeshi, sehemu kubwa ya wachezaji wake wapo kwenye ajira za kudumu.

Ubora wa ligi hiyo miaka ya nyuma ulitokana na wafadhili kujitoa kwa kila hali kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi wakiwemo wachezaji kutoka Bara akiwemo Dua Said, Edibily Lunyamila, Victor Bambo ambao waliichezea Malindi na wachezaji wengine wawili kutoka Bulgaria waliolipwa mishahara kwa dola. Pia timu hiyo ilikuwa na jeuri ya kuwachukua wachezaji kutoka Zambia.

Small Simba ni timu ya mtaani, iliyoibuka miaka ya 1960, awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sunderland na mwaka 1970 waliamua kubadilisha jina na kuitwa Small Simba.

Hata hivyo, timu hiyo haina uhusiano wala urafiki wowote na Simba SC ya Bara, huku ikielezwa kuwa Simba ya Bara ina urafiki mkubwa na Kikwajuni.

Small Simba nayo ilitamba na kuwavutia wachezaji kutoka Bara akiwamo kipa James Kisaka ambaye kwa sasa ni marehemu, Innocent Haule na Shaaban Mussa ambao pia waliwahi kuichezea Simba ya Dar es Salaam.

Tofauti na timu nyingine zilizokuwa na wafadhili, Small Simba ilikuwa timu ya wakereketwa, haikuwa na mfadhili mwenye nguvu na zaidi ilikuwa ikijiendesha yenyewe chini ya kocha wao Abdulghan Msoma.

Miongoni mwa mambo ya kukumbukwa kwa timu za Zanzibar kutamba Bara, ni pamoja na timu ya Malindi kuwahi kutwaa ubingwa wa Muungano ikiifunga Pamba katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Katika mechi hiyo ilichezwa mwaka 1989, Malindi iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lakini kwa Zanzibar imewahi kutwaa taji la ligi mwaka 1991 na 1992.

Pia, ilishikiri Kombe la CAF mwaka 1995 na kuishia hatua ya nusu fainali, mafanikio ya Malindi kwa wakati huo yalisaidia kuipandisha chati Tanzania katika viwango vya Fifa.

Kiwango cha Malindi kwa wakati huo kilisaidia kuipandisha chati Tanzania katika viwango vya Fifa ikawa nafasi ya 65 duniani. Rekodi ambayo haijaweza kuvunjwa hadi sasa.

Ni mwaka huo huo wa 1995 ambao Zanzibar Heroes iliibuka kidedea katika Kombe la Chalenji nchini Uganda.

Small Simba ambayo kwa sasa inashiriki Ligi Daraja la Pili iliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mwaka 1984 na 1988 na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Kujitoa kwa wafadhili hao kulianza kupunguza morali ya soka visiwani humo huku idadi ya wachezaji wa kigeni nayo ikaanza kupungua kadiri siku zilivyokwenda na hadi sasa hakuna wachezaji wa kigeni wenye kutoa upinzani, soka limebaki kuwa na watu wa visiwani humo pekee.

Kwa sasa soka la Zanzibar badala ya kupanda linazidi kudidimia na kupoteza ule ushindani wa miaka ya nyuma.

Gazeti la Mwanaspoti limebaini baadhi ya mambo ambayo ni kiini cha soka la visiwani humo kushuka huku mchezo huo ukipoteza mvuto kwa mashabiki wake.

Mwanaspoti limezungumza na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi, makocha na wachezaji wa zamani ambao wameelezea sababu mbalimbali za kushuka kwa soka la Zanzibar.

 

Siasa

Wakati timu kongwe zikipata wadhamini waliopandisha morali ya soka, siasa za vyama vingi zilianza kupamba moto, inaelezwa kwamba hiyo ndiyo sababu hasa ya soka kuanza kuporomoka.  Wadau wengi waliingia kwenye siasa na kuendesha soka kisiasa.

Inadaiwa kwamba Noushad aliamua kujitoa kuisaidia timu hiyo baada ya Jimbo la Malindi lililokuwa chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchukuliwa na CUF ingawa hakuwa na nia ya kugombea ubunge lakini alitaka jimbo hilo libaki mikononi mwa CCM.

 

Hii ni sehemu ya kwanza ya makala haya ambayo yanaelezea kupanda na kushuka kwa soka la Zanzibar,  usikose sehemu ya pili, Jumatatu.

 

 

 

 

 

 

 

Mmoja wa viongozi wa Malindi ambaye pia aliisaidia timu hiyo hadi kupanda daraja mwaka 1987, Amir Saleh anaeleza: “Kwa upande wetu tunashukuru sana Noushad aliondoka akiwa ametuachia vitega uchumi, tunaingiza japo fedha kidogo ingawa haikidhi mahitaji ya klabu.

“Tangu aondoke yeye maisha ya timu yamekuwa mabaya, tupo kwenye ligi lakini tunaenda hivyo hivyo, mambo ya siasa yalichangia kwa kiasi fulani kushusha soka letu.”

Kwa upande wake mwanasoka mkongwe wa Zanzibar, Abdulla Juma maarufu Abdul Wakat Jumaa’ anasema:

“Visiwani hapa siasa imetawala mpaka kwenye michezo, binafsi niliacha hata kwenda uwanjani kwa sababu hakuna mambo ya maana yanayoendelea, watu hawazungumzii michezo badala yake wanazungumza siasa.

“Ukiangalia hata viongozi wetu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) wapo kisiasa zaidi, kwa mfumo huo soka haliwezi kukuwa kwani walio wengi wanaingia kwa lengo la kupata umaarufu ili waingie kirahisi kwenye siasa, ni jambo ambalo linakatisha tamaa ukizangatia Zanzibar ni sehemu ambayo ina wachezaji wengi wenye vipaji.”

Abdul Wakat anakwenda mbali zaidi kwa kusema: “Hata wafadhili wa timu nadhani nao waliingia kwa ajili ya kupata urahisi wa kuingia kwenye vyama vya siasa, sidhani kama walikuwa na nia njema.

Itaendelea Jumatatu ijayo…