Shime: Uganda imetupa maswali magumu

Muktasari:
- Twiga Stars kesho itacheza mchezo wa nne na wa mwisho kwenye mashindano ya Wanawake ya Cecafa yanayoendelea katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam dhidi ya Kenya ambayo haijapoteza mchezo wowote.
KOCHA wa Timu ya Taifa 'Twiga Stars', Bakari Shime amesema ushindi dhidi ya Uganda jana wa mabao 2-0 umewapa maswali magumu ya kujiuliza kuelekea mechi ya kesho, Juni 21 dhidi ya Kenya.
Twiga Stars kesho itacheza mchezo wa nne na wa mwisho kwenye mashindano ya Wanawake ya Cecafa yanayoendelea katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam dhidi ya Kenya ambayo haijapoteza mchezo wowote.
Shime aliongeza kuwa Uganda iliwapa mchezo mgumu na waliwaona Kenya walivyocheza, hivyo wamefanyia kazi baadhi ya makosa ikiwemo ya kupoteza nafasi.
"Matarajio yetu ni kucheza vizuri mechi ya leo (jana), tumeona baadhi ya upungufu ikiwemo kupoteza nafasi, na kwa ubora wa Kenya tunapaswa kuwa makini," amesema Shime na kuongeza:
"Beki wetu Ester Maseke aliumia mechi iliyopita, bado hatuna uhakika kama atacheza lakini tutajaribu kumfuatilia, ikishindikana tutaangalia namna nyingine."
Timu hizo zinakutana kila moja ikiwa imeshinda mechi zote tatu na hazijaruhusu bao, huku Kenya ikifunga mabao 11 na Tanzania ikitikisa nyavu mara 12.
Twiga Stars ilianza na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Sudan Kusini, ikaitandika Burundi mabao 6-0, na mechi ya juzi ikishinda kwa 2-0 dhidi ya Uganda.
Ikumbukwe Zanzibar ilikuwa timu ya kwanza kuandika historia kwenye mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 1986 kwa kuchukua ubingwa.
Hata hivyo, mashindano hayo hayakuendelea kwa takriban miaka 30, ingawa kulikuwa na jitihada za kuyarudisha, na mwaka 2007 yalifufuliwa yakipigwa Zanzibar, lakini baadaye yakafutwa na hayakuchezwa tena.
Mwaka 2016 yalirejeshwa tena na Uganda ikawa mwenyeji, na Tanzania iliibuka bingwa wa mashindano hayo, huku mwaka 2018 Tanzania ikitetea ubingwa na kutwaa kwa mara ya pili mfululizo.
Ubingwa wa mara mbili mfululizo uliifanya Tanzania mwaka 2019 kupewa heshima ya kuwa mwenyeji. Hata hivyo, ilishindwa kutetea mara ya tatu baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Kenya.
Mwaka 2021 hayakuchezwa kutokana na marekebisho ya uwanja yaliyokuwa yakiendelea nchini Djibouti ambako yalipangwa kufanyika, na msimu uliofuata Uganda ikanyakua taji hilo baada ya kuichapa Burundi mabao 3-1 kwenye fainali iliyopigwa mjini Jinja, Uganda.
MSIMAMO P W D L F GA Pts
1.Tanzania 3 3 0 0 12 0 9
2.Kenya 3 3 0 0 11 0 9
3.Uganda 4 1 0 3 5 7 3
4.Burundi 3 1 0 2 1 9 3
5.South Sudan 3 0 0 3 0 13 0
WAFUNGAJI
5 Opah Clement (Tanzania)
3 Sylivia Kabene (Uganda)
Martha Emedot (Kenya)
2 Faith Mboya (Kenya)
Diana Msewa (Tanzania)
1 Namuleme Zaina (Uganda)
Esperance Habonimana (Burundi)
Clara Luvanga (Tanzania)
Nalugya Shamirah (Uganda)