Shija arudisha fomu, alia 'endorsement'

Muktasari:
- Shija ambaye ni mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), amesema katika mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu, amekumbana na changamoto ya kukosa uidhinishwaji kutoka kwa wajumbe wa mkutano mkuu.
Mgombea urais kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Shija Richard amesema licha ya kurudisha fomu, lakini kinachomliza ni changamoto ya kukosa uidhinishwaji (endorsement).
Shija ambaye ni mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), amesema katika mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu, amekumbana na changamoto ya kukosa uidhinishwaji kutoka kwa wajumbe wa mkutano mkuu.
Mgombea huyo amesema kwa hatua hiyo anakusudia kufungua kesi katika kamati mbili za TFF ile ya maadili na ya rufani za uchaguzi.
"Nimerudisha fomu mama mnavyoona, lakini niungane na wengine ambao wameonyesha kukosa hizi endorsement (uidhinishwaji). Mimi ni mzoefu wa uchaguzi wa TFF na nimewahi mpaka kufikia hatua ya kupigiwa kura," amesema Shija.
"Kila unayemgusa kwenye watu 47 unaambiwa zimeshatoka. Sasa kila mmoja analia hizi zimekwenda wapi? Nilichokuja kugundua ni kwamba kuna mgombea mwenzetu mmoja amezichukua zote.
"Hatuwezi kuwa na uchaguzi wa huru kwa njia kama hii. Mimi binafsi nasema najipanga kwenda kushtaki haya kamati ya maadili kwa kuwa uidhinishwaji ulitakiwa kufanyika kuanzia ile siku ya kuchukua fomu ilipoanza.
"Nitapeleka pia malalamiko Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, ili kupinga mambo haya. Hakuna usawa lakini pia nitakwenda mpaka Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ambao TFF ipo chini ya chombo hicho."