Sh100 milioni kutumika Chemchem Cup Babati

Muktasari:
- Mashindano hayo yanafanyika kwa msimu wa tisa huku yakiwa na lengo la kupiga vita ujangili wa wanyama pori pamoja na kuibua vipaji vya Soka kwa vijana
Arusha. Jumla ya Sh100 milioni zimepangwa kutumika kwenye mashindano ya soka ya Chemchem Cup ambayo yanayoendelea katika uwanja wa Mdori iliyopo wilayani Babati Mkoa wa Manyara.
Mashindano hayo yanafanyika kwa msimu wa tisa sasa yakiwa na lengo la kupiga vita ujangili wa wanyama pori pamoja na kuibua vipaji vya soka kwa vijana.
Katibu wa Chemchep Cup, John Bura amesema wanatazamia kutumia Sh100 milioni ambazo zitajumlisha zawadi kwa washindi, lakini pia fedha za kuendesha mashindano.
Amesema mashindano ambayo yamedhaminiwa na taasisi ya Chemchem iliyowekeza shughuli za Utalii na Uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya jamii ya wanyamapori Burunge ilianza kwa kushirikisha timu 31 za wanaume, vijana chini ya umri wa miaka 18 na wanawake.
Ameongeza kuwa kwa sasa wako katika hatua ya robo fainali ambayo ina timu sita sita za wanaume na vijana huku wanawake zikiwa timu tatu na itachezwa kwa mtindo wa Ligi kupata timu ambazo zitatinga nusu fainali na fainali yenyewe.
Alitaja baadhi ya timu ambazo zimetinga robo fainali kuwa ni Macklion, Macedonia, Mdori FC, Olasiti FC, Manyara FC na Maweni FC, Wanawake ni Mwada Queen, Maweni Queen na Majengo Mdori.
Kwa upande wa vijana chini ya umri wa miaka 18 ni Mwada FC ,Ngolei FC, Magara FC, Mejengo FC, Scopion na Maweni.
Mkurugenzi wa ChemChem Association, Fabia Bausch amesema michuano hiyo tangu imeanzishwa imekuwa na faida kubwa kushirikisha jamii katika uhifadhi.
Amesema mwaka huu kauli mbiu ni ‘Kupiga Vita ujangili wa Twiga’ na kuongeza kuwa ushindani umekuwa ni mkubwa kutokana na timu shiriki.
Mwenyekiti wa michuano hiyo, Erasto Belela amesema mshindi wa kwanza atapewa zawadi ya Sh2.5 milioni, wa pili Sh1.5 milioni wa tatu milioni moja ambapo kwa upande wa Wanawake bingwa atapata Sh1.5 milioni,mshindi wa pili million Moja na mshindi wa tatu Sh500,000.
Upande wa vijana U-18 mshindi atapata milioni Moja wa pili Sh600,000 na wa tatu Sh400,000 ambapo timu zote zilipewa seti ya jezi na mipira kwa ajili ya maandalizi.