Shafii Lumambo anasikilizia Uturuki

Muktasari:
- Nyota huyo alisema timu hiyo, ambayo awali ilikuwa inaitwa Tuzlaspor, iliuzwa na kununuliwa na chama la sasa, hivyo bado hajafahamu hatma yake kama atasalia ama ataondoka.
KIUNGO mshambuliaji wa Kitanzania anayekipiga Beykoz Anadolu Spor ya Uturuki, Shafii Omary Lumambo amesema bado hajasaini mkataba mpya na chama hilo, zikiwa zimesalia siku chache kumaliza mkataba wa awali unaotamatika Juni 30.
Nyota huyo alisema timu hiyo, ambayo awali ilikuwa inaitwa Tuzlaspor, iliuzwa na kununuliwa na chama la sasa, hivyo bado hajafahamu hatma yake kama atasalia ama ataondoka.
Akizungumza na Mwanaspoti, alisema msimu huu ambao ni wa pili kwake ulikuwa na ushindani na kubwa zaidi ni majeraha ya nyama ya paja aliyoyapata ambayo yalimrudisha nyuma.
“Timu yetu iliuzwa, walionunua wakabadilisha jina. Wachezaji waliokuwa wanawahitaji walibaki nao, mmoja wapo ni mimi pia, lakini hadi sasa bado hatujazungumza mkataba mpya.”
“Kila timu ina malengo yake, hivyo kama sitakuwa sehemu ya kikosi hicho msimu ujao basi nitaangalia utaratibu mwingine. Nimepata baadhi ya ofa kutoka nje pia.”
Msimu wa kwanza 2023/24, mchezaji huyo mwenye miaka 20 alikuwa miongoni mwa waliotoa mchango mkubwa katika ligi ya vijana. Katika michezo 22, alihusika na mabao 24, akifunga 13 na kuasisti 11.