Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgunda ashikilia hatma ya Kagere

KAGERE Pict

Muktasari:

  • Kagere anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyetwaa Tuzo ya Mfungaji Bora na kuitetea katika Ligi Kuu Bara yupo Namungo aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Singida Fountain Gate iliyomsajili kutokea Simba aliyoitumikia kwa misimu minne mfululizo kati ya 2018-2022.

HATMA ya mshambuliaji mkongwe wa Namungo, Meddie Kagere 'MK14' kuendelea kuwepo katika kikosi hicho kwa msimu ujao ipo kwa kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda baada ya nyota huyo aliyefanya makubwa kwenye soka la Tanzania, mkataba alionao kumalizika.

Kagere anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyetwaa Tuzo ya Mfungaji Bora na kuitetea katika Ligi Kuu Bara yupo Namungo aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Singida Fountain Gate iliyomsajili kutokea Simba aliyoitumikia kwa misimu minne mfululizo kati ya 2018-2022.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema ni kweli mchezaji huyo amemaliza mkataba na kikosi hicho, ingawa suala la kubaki au kuondoka itategemea na mapendekezo ya benchi lao la ufundi chini ya kocha Mgunda.

"Ni kweli Kagere mkataba wake umeisha ila suala la kuondoka au kubaki itategemea na benchi la ufundi, ni mchezaji mzuri na mzoefu ambaye amesaidia kujenga morali ya wachezaji wadogo kupambana na kufikia malengo yetu kijumla," alisema Ally.

Bosi huyo alisema mambo yote yanayohusu mchezaji kubaki au kuondoka wataachia jukumu hilo benchi la ufundi na hawatokuwa tayari kuwaingilia, kwani lengo lao kubwa watakaolifanyia kazi ni ripoti ya mapendekezo ya nyota wanaohitajika kikosini.

Nyota huyo raia wa Rwanda wakati anaondoka Simba, aliweka rekodi tamu kwa mastaa wa kigeni katika Ligi Kuu Bara ambayo imeendelea kuishi hadi leo, kwani licha ya wachezaji wengi waliokuwa bora na wazoefu kucheza ila wameshindwa kuifikia.

Kagere alitua Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya msimu wa 2018-2019 na kufunga mabao 23 na kuipiku rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ya wachezaji wa kigeni kufunga mabao mengi msimu mmoja alipofunga 21 msimu wa 2015-2016.

Msimu wa pili kwa staa huyo akiwa na Simba pia, alifunga mabao 22 na kutetea tuzo ya mfungaji bora ikiwa pia ni rekodi kwani, haikuwahi kutokea kwa mchezaji yeyote iwe mzawa au wa kigeni kutwaa tuzo ya ufungaji bora mara mbili mfululizo.

Baada ya hapo MK14 akaachana na kikosi cha Simba na kujiunga na Singida Big Stars msimu wa 2022-2023 na aliendelea kuonyesha kiwango bora baada ya kufunga mabao manane, kisha msimu wa 2023-2024 akiwa Namungo akaifungia mabao mawili.

Licha ya rekodi hizo tamu, ila nyota huyo anaandamwa na ukame wa mabao, kwani mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara kufunga bao ni ile ya Februari 24, 2024, dhidi ya KMC, ambayo kikosi cha 'Wauaji wa Kusini' kilitoka sare ugenini ya mabao 2-2.