Sey:Kutinga makundi si kazi nyepesi

Muktasari:

Namungo imetinga hatua ya makundi michuano ya Caf, hilo limewapa kicheko wachezaji wa timu hiyo, kuandika rekodi itakayokumbukwa miaka nenda rudi kama anavyosimulia Stephen Sey.
 

STRAIKA wa Namungo FC, Stephen Sey  amesema ni faraja kwake kuisaidia timu kutinga hatua ya makundi ya  Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa imeshiriki kwa mara ya kwanza.

 Sey ameliambia Mwanaspoti online, kwamba wameandika rekodi yakukumbukwa ushujaa wao wakupambana kwenye nyakati ngumu na nyepesi timu kutinga hatua ya makundi, huku akiwa amefunga mabao matano katika mechi zote.

"Haikuwa kazi rahisi, tumefanya kitu cha kishujaa kuifikisha timu hatua ya makundi, imetupa ujasiri na moyo wa kuendelea kupambana kwa hatua ya mbele zaidi, tunaamini inawezekana kufanya makubwa zaidi,"amesema.

Amesema michuano ya Caf sio rahisi kwani wamekutana na timu ambazo zinatumia akili nyingi kutafuta matokeo na kwamba kosa moja ni kosa, tofauti na ligi ya ndani ambapo mchezaji anaweza akapata nafasi nne akatumia moja kupata bao.

"Michuano ya Caf mchezaji akipata nafasi moja ya kufunga anafunga, beki akikosea basi ndio amekosea, inahitaji akili kubwa, maarifa na umakini wa hali ya juu ili kupata matokeo, ndio maana nasema sio rahisi sisi kutinga hatua ya makundi," amesema.

Namungo imefika hatua hiyo kutokana na kushinda mechi dhidi ya  Al Rabita mabao  3-0,kisha wakapita kiulaini mchezo wa marudio  uliopangwa upigwe  Desemba 06/12/2020 kufutia Al Rabita kutotimiza vigezo vya maandalizi ya mechi kisha  Namungo ikapewa ushindi wa mezani.

Namungo walivuka hatua ya pili walipokutana na  Hilal Obayed wakishinda nyumbani kwa mabao  2-0,  mechi ya marudiano ilipigwa mabao 2-1 wakivuka kwa jumla ya mabao 3-2.

Timu hiyo pia ikapata zali lingine l;a kucheza mechi mbili nyumbani dhidi ya 1º de Agosto wakishinda mabao 6-2 katika mechi ya kwanza huku mchezo wa pili wakipoteza kwa mabao 3-1 na kutinga hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 7-5.