UCHAMBUZI: KOCHA Mkwasa, Baraza wanasafiri boti moja

Saturday February 27 2021
Mkwasapic
By Charles Abel

LIGI Kuu Tanzania Bara ipo katika mzunguko wa pili ambapo Yanga inaongoza msimamo ikiwa imekusanya pointi 49 baada ya kucheza mechi 21 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 42 ilizokusanya katika michezo 18.

Ni wazi kwamba kwa namna msimamo wa Ligi Kuu ulivyo, timu za Simba na Yanga ndio washindani hasa wa ubingwa kwani kuna pengo kubwa la pointi baina yao na Azam FC inayoshika nafasi ya tatu.

Ukiachana na upande wa ubingwa vita na ushindani mkubwa uliopo kwa sasa ni upande wa timu zinazopigania kutoshuka daraja ambazo kila moja imekuwa ikipambana vilivyo kuhakikisha inajiondoa katika nafasi mbaya zinazoweza kuigharimu mwishoni mwa msimu.

Kwa namna msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ulivyo, kuanzia timu ya Prisons iliyoko nafasi ya nane hadi Mwadui inayoshika mkia, yoyote inaweza kushuka daraja ikiwa haitachanga vyema karata zake.

Hii ni kwa sababu timu nne zitakazoshika mkia zitashuka moja kwa moja na mbili ambazo zitamaliza katika nafasi ya 13 na 14 zitacheza mechi za mchujo (play offs) dhidi ya timu za Ligi Daraja la Kwanza ili kupambania nafasi ya kubaki Ligi Kuu kwa mujibu wa kanuni.

Lakini zipo timu ambazo zinaonekana zipo katika nafasi salama kutokana na idadi ya pointi ambazo zimekusanya hadi sasa lakini pia kiwango bora ambacho zimekuwa nacho katika siku za hivi karibuni, kiasi cha kutia matumaini kwamba zitafanya vizuri katika idadi kubwa ya mechi zao.

Advertisement

Mfano wa timu hizo ni Biashara United ya mkoani Mara na wenzao wa Ruvu Shooting kutoka pale Mlandizi mkoani Pwani.

Hawa Biashara United kwa sasa wako nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa wamekusanya pointi 35 ambazo ni mbili tu nyuma ya Azam FC walio kwenye nafasi ya tatu.

Silaha yao kubwa imekuwa ni uwanja wao wa nyumbani wa Karume mkoani Mara ambako katika michezo 11 waliyocheza hapo wamepoteza miwili tu tena dhidi ya Simba na Yanga, kutoka sare mbili na kuibuka na ushindi katika mechi saba

Ukiondoa Biashara United, kuna Ruvu Shooting nao ambao wamekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu wakijikita katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi na pointi zao 31 walizokusanya.

Kama ilivyo kwa Biashara United ambayo imekuwa tishio pindi iwapo nyumbani mwake ndivyo ilivyo kwa Ruvu Shooting ambayo imekuwa haipotezi mechi kirahisi pindi inapokuwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Mabatini.

Katika mechi tisa ilizocheza kwenye uwanja huo, imepoteza mechi moja tu huku ikitoka sare mara tatu na imeibuka na ushindi mara tano na kupoteza mchezo mmoja.

Pamoja na ubabe wao nyumbani, Ruvu Shooting na Biashara United pia zimekuwa zikivuna pointi katika viwanja vya ugenini jambo ambalo huwa ni nadra kutokea katika ligi yetu.

Hata hivyo, nyuma ya mafanikio ya Biashara United na Ruvu Shooting msimu huu wako watu wawili ambao ni Boniface Mkwasa na Francis Baraza wanaozinoa timu hizo mbili.

Hawa wameweza kujenga vikosi vya wachezaji wenye ushindani lakini pia wanaocheza kwa nidhamu kubwa ndani ya uwanja wakifanyia kazi kwa ufasaha maelekezo ambayo wamekuwa wakipewa na benchi lao la ufundi

Lakini pia wameweza kuboresha kiwango cha mchezaji mmojammoja na kufanya wengi wao wawe na muendelezo wa kucheza vizuri tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Yote hayo yanafanyika huku Biashara United na Ruvu Shooting zikiwa zinaendeshwa kwa bajeti ndogo ya fedha tofauti na ilivyo kwa timu kama Simba, Yanga na Azam.

Hazina uwezo wa kusajili wachezaji wa gharama kubwa lakini wale ambao zinawapata kwa bajeti yao, wanajengwa na kuandaliwa vizuri na makocha hao wawili na kuwafanya waweze kumudu ushindani wa ligi.

Mkwasa na Baraza wamekuwa wakitumia muda mwingi kushughulika na masuala ya kiufundi kwa ajili ya kuziimarisha timu zao na wanaonekana kujiweka kando na mambo yasiyowahusu ambayo ni ama ya kiutawala au kiuongozi

Mwisho wa yote imewasaidia wao wenyewe kupandisha thamani na hadhi yao licha ya kufundisha klabu ndogo hapa nchini na hapana shaka kwa sasa wamekuwa bidhaa adimu sokoni

Advertisement