Vipigo vikali Kariakoo Derby miaka 20 ya Mwanaspoti

ACHANA na vipigo vizito vya mwaka 1968 na kile cha 1979 wakati Simba na Yanga zilipotiana aibu, unaambiwa katika kipindi cha miaka 20 ya uwepo wa Gazeti la Mwanaspoti, limeshuhudia idadi kubwa ya mechi za watani wa jadi, Yanga na Simba ambazo zilikuwa na matokeo tofauti.

Kwa wanaokumbuka mwaka 1968 Yanga ilizindua kipigo kikubwa dhidi ya Simba walipoinyoa mabao 5-0 kabla ya Simba kulipa kisasi 1979 kwa kuikandika Yanga mabao 6-0 ambayo hayajarudi mpaka leo hii.

Hata hivyo tuachane na huko, ndani ya miaka 20 ya Mwanaspoti mashabiki wa soka wameshuhudia vipigo vya mechi za watani hao zenye mabao mengi.

Zipo mechi ambazo Yanga iliibuka na ushindi na mechi nyingine ilipoteza mbele ya Simba lakini pia kuna michezo ambayo timu hizo zilitoka sare. Lakini zipo pia mechi za watani wa jadi ambazo timu moja ilipokea kipigo kikubwa kutoka kwa nyingine jambo ambalo upande mmoja unabaki na kumbukumbu ya kuvutia huku mwingine ukibaki na historia ya maumivu.

Gazeti hili linakuletea orodha ya mechi za watani wa jadi , Simba na Yanga kuanzia mwaka 2001 wakati gazeti hili linaanzishwa hadi mwaka huu ambazo timu mojawapo ilipokea kichapo cha haja.

Simba 4-1 Yanga (2002)

Kichapo cha kwanza kikubwa katika mechi za watani wa jadi mara baada ya gazeti la Mwanaspoti kuanzishwa kilikuwa ni kile cha mabao 4-1 ambacho Yanga ilikipata katika mchezo wa fainali ya Kombe la Tusker uliofanyika Machi 31, 2002.

Mark Sirengo aliitanguliza Simba kwa kuifungia bao la mapema katika dakika ya tatu ya mchezo lakini katika dakika ya 16, Sekilojo Chambua aliisawazishia Yanga bao hilo.

Mchezo huo nusura uvunjike katika dakika ya 32 ya mchezo baada ya Madaraka Selemani kuifungia Simba bao la pili ambalo Yanga walililalamikia kuwa mfungaji alishika mpira kabla ya kupachika bao hilo jambo lililopelekea kutokea kwa vurugu kubwa ingawa baadaye zilitulia na mechi kuendelea.

Katika mechi hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, mabao mengine ya Simba yalifungwa na Sirengo katika dakika ya 76 na Emmanuel Gabriel mnamo dakika ya 83.

Yanga 3-0 Simba (2003)

Baada ya kufungwa 4-1 kwenye Fainali ya Kombe la Tusker, Yanga waliingia msituni kujipanga na mwaka mmoja baadaye walilipa kisasi kwa Simba baada ya kuichapa mabao 3-0 katika mechi ya Ngao ya Hisani iliyochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Aprili 20, 2003.

Mabao ya ushindi ya Yanga katika mechi hiyo yalifungwa na Kudra Omary, Heri Morris na Salum Athuman.

Simba 4-3 Yanga (2010)

Ulikuwa ni mchezo wa kufunga msimu wa Ligi Kuu 2009/2010 ambao Simba waliibuka washindi kwa kuichapa Yanga jumla ya mabao 4-3, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa (Benjamin Mkapa) jijini Dar es Salaam.

Mabao manne ya Simba walifungwa na Musa Mgosi aliyepachika mabao mawili, Hillary Echesa na Uhuru Selemani wakati yale ya Yanga, mawili yalifungwa na Jerry Tegete huku lingine likifungwa na Athuman Iddi ‘Chuji’

Simba 5-0 Yanga (2012)

Kipigo kikubwa zaidi katika mechi za watani wa jadi ambacho kiliwahi kutokea katika kipindi cha miaka 20 ya Mwanaspoti ni kile cha mabao 5-0 ambacho Yanga ilikipata kutoka kwa Simba mnamo Mei 6, 2012 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Emmanuel Okwi alifunga mabao mawili katika mechi hiyo huku mengine matatu yakifungwa na Patrick Mafisango, Juma Kaseja na Felix Sunzu.

Simba 3-1 Yanga (2013)

Wakati kidonda cha mwaka 2012 kwa Yanga hakijapoa, ilijikuta ikichapwa mabao 3-1 mwaka mmoja uliofuata katika mchezo wa kusaka bingwa wa shindano la Nani Mtani Jembe uliochezwa Disemba 21, 2013. Amissi Tambwe aliifungia Simba mabao mawili katika mchezo huo na bao lingine moja lilifungwa na Awadh Juma ‘Maniche’.

Simba 4-1 Yanga (2020)

Ilipita muda mrefu bila mashabiki kuona kipigo kikubwa kwenye mechi ya watani wa jadi lakini mwaka jana Julai 12, Simba waliichapa Yanga kwa mabao 4-1 katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Gerson Fraga na Luis Miquissone kila mmoja aliifungia bao Simba wakati upande wa Yanga, bao lao la kufutia machozi lilipachikwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’.