Sey kuivaa Azam

DODOMA Jiji imebakiza mechi tisa za kujinusuru na janga la kushuka daraja na jukumu la kuhakikisha wanatimiza hilo limeachiwa kwa nyota wake mpya iliyemsajili katika dirisha dogo la usajili, Stephen Sey ambaye bado hata hajaanza kuitumikia kazi.

Sey ambaye alinaswa na Dodoma Jiji akiwa huru, bado hajaichezea timu hiyo kwenye ligi kutokana na kuchelewa kukamilisha vibali lakini ataanza rasmi kuonekana uwanjani katika mchezo unaofuata wa timu yake dhidi ya Azam FC, katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Ijumaa hii katika Uwanja wa Azam Complex.

Kocha msaidizi wa Dodoma Jiji FC ambayo juzi ilichapwa bao 1-0 na Simba, Kassim Liogope aliliambia gazeti hili kuwa kuanza kucheza kwa Sey kutaipa unafuu mkubwa timu yake kutokana na uwezo wa kufumania nyavu ambao Mghana huyo anao pamoja na uzoefu wake.

“Sey ni mchezaji muhimu lakini tumechelewa kumtumia kuna mambo yalikuwa hayajakaa sawa lakini sasa ataonekana uwanjani katika mechi zinazofuata. Tuna imani ataiimarisha kwa kiasi kikubwa safu yetu ya ushambuliaji kwa vile ni mchezaji mzuri na mwenye uwezo mkubwa wa kufunga.

“Ni kweli tuna changamoto katika safu ya ushambuliaji ambayo tunapambana kuirekebisha. Ukitazama mechi tulizocheza siku za hivi karibuni, tumekuwa tukicheza vizuri lakini tumekuwa tukipoteza nafasi nyingi hivyo uwepo wa Sey utaongeza kitu kikosini,” alisema Liogope.

Dodoma Jiji FC imefunga mabao 14 tu katika mechi 21 za Ligi Kuu msimu huu, huku mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika kikosi chao akiwa ni Collins Opare aliyepachika mabao manne.