Serengeti Girls iungwe mkono

WADAU wa soka wameombwa kuiunga mkono timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’ inayotarajia kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika mwezi ujao nchini India.

Kocha wa timu hiyo, Bakari Shime alisema wachezaji wanakwenda kuipeperusha bendera ya Tanzania hivyo wapewe moyo na ari ya kupambana ili wakaonyesha namna taifa lao lilivyo na vipaji vikubwa.

Kiufundi alisema wachezaji anawaandaa vizuri wanafanya mazoezi Uwanja wa Uhuru, ili kujiweka fiti kimwili na kiakili kujiweka tayari kwenda kushindana.

“Naamini wakiungwa mkono na kupewa moyo, kwenye akili zao watakuwa wanatembea na maneno ya Watanzania wanahitaji kuona wanaipeperusha bendera ya taifa lao kwa ushujaa wa kufanya makubwa kwenye michuano mikubwa duniani,” alisema na kuongeza;

“Kama kocha nawapa mbinu za namna watakavyokuwa bora dhidi ya wapinzani, nawaamini wana uwezo mkubwa wa kuonyesha vipaji vyao ndio maana wamefika hatua hiyo ya kwenda kushiriki mashindano hayo.”

Alisema wachezaji hao wamekuwa kioo kwa mabinti wengine kuona soka la sasa ni ajira na fursa ya kusafiri nchi mbalimbali duniani.

“Michuano ya Kombe la Dunia ni mikubwa, mabinti wengine watakapokuwa wanaifuatilia watakuwa wanapata moyo wa kuona ni kazi inayoheshimika na watavipambania vipaji vyao, jambo zuri zaidi ni jinsi ambavyo serikali inawaunga mkono,”alisema.