Serengeti Boys kamili gado kuivaa Rwanda

Muktasari:
- Serengeti Boys imepanga kuitumia michuano hiyo kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Dar es Salaam Aprili 14 hadi 28, mwaka huu.
Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ’Serengeti Boys’ kesho itashuka uwanjani kuvaana na Rwanda katika michuano ya kirafiki inayoshirikisha timu tatu ikiwemo Cameroon.
Serengeti Boys inacheza na Rwanda ikiwa na morali baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Camroon katika mchezo uliopita.
Hata hivyo, timu hiyo itaingia uwanjani bila mshambuliaji nyota Kelvin John aliyeumia katika mchezo uliopita.
Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema amewaandaa vyema wachezaji kupata ushindi dhidi ya Rwanda.
“Ukiangalia mchezo uliopita tulipata matokeo mazuri lakini bado kulikuwa na makosa mengi ikiwemo ukosefu wa umakini kwa wachezaji wangu pale tunapokuwa na mpira na hata tunapokuwa hatuna mpira.
"Kadri tutakavyokuwa tunacheza mechi za kirafiki tunagundua wapi tunahitaji kusahihisha makosa na kuongeza nguvu, kubwa tunataka tuimarike katika ufungaji wa mabao,"alisema Mirambo
Serengeti Boys imepanga kuitumia michuano hiyo kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Dar es Salaam Aprili 14 hadi 28, mwaka huu.