Samatta mbioni kurudi England

RIPOTI kutoka Ubelgiji zinamhusisha mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ kutua Cardiff City ya Ligi Daraja la Kwanza England ‘Championship’.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 29 ameonyeshewa malango wa kutokea huko Uturuki kwenye klabu yake ya Fenerbahce baada ya kutokuwa kwenye mipango ya kocha mpya wa kikosi hicho, Jorge Jesus, raia wa Ureno.

Mwandishi wa habari wa Ubelgiji, Sacha Tavolieri ameripoti kuwa Cardiff wapo kwenye mazungumzo juu ya uwezekano wa kumchukua mshambuliaji huyo kwa mkopo.

Hata hivyo, zipo ripoti nyingine kwamba Samatta huenda akarejea katika klabu yake ya zamani ya Genk ya Ubelgiji, ambako alitengeneza jina lake kwa kufunga mabao 75 katika michezo 191 kati ya mwaka 2016 na 2020.

Kocha wa Cardiff City, Steve Morison bado hajafanya uamuzi madhubuti kuhusu wanaoingia na wanaoondoka huku akitaja kuwa mwezi ujao utakuwa mgumu.

The Bluebirds wana mechi tano ngumu mbele yao kabla ya dirisha la usajili kufungwa Septemba 1. Morrison ameleta wachezaji 14 lakini bado anaweza kuongeza wengine kabla ya tarehe ya mwisho.

Baada ya mchezo dhidi ya Reading, alisema: “Ni mwezi wa ajabu. Unatazama kikosi na kufikiria, ‘Je, ninaleta mtu? Je, niruhusu mtu aende? Kuna tofauti nyingi, unapofika mwisho wa dirisha la usajili.”