Samatta bado moja kurudi Ligi ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:
- Chama la Samatta, PAOK linahitaji ushindi wa pointi tatu kwenye mechi mbili zilizosalia ili kushiriki michuano hiyo mikubwa na yenye hadhi zaidi Ulaya msimu ujao.
NAHODHA wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', Mbwana Samatta anasubiri ushindi wa mechi moja ili kuweka rekodi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya pili katika historia ya maisha yake ya soka.
Chama la Samatta, PAOK linahitaji ushindi wa pointi tatu kwenye mechi mbili zilizosalia ili kushiriki michuano hiyo mikubwa na yenye hadhi zaidi Ulaya msimu ujao.
Samatta ameshaweka rekodi kadhaa tangu aanze kucheza soka la kulipwa ikiwamo kuibuka mchezaji bora wa Afrika na mfungaji bora wa KRC Genk ya Ubelgiji alikomaliza na mabao 20 msimu 2018/19 na kuwa Mtanzania wa kwanza kushiriki michuano hiyo na sasa anasaka rekodi nyingine.
PAOK inashiriki ligi hiyo ya Super League inayohusisha timu nne za juu za Ligi Kuu ya Ugiriki, zitakazoamua bingwa na hucheza zenyewe kwa zenyewe mechi sita na ya kwanza na ya pili ndizo zinashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na ya tatu na nne zinakwenda Europe League.
Hadi sasa PAOK imecheza mechi nne ikishinda tatu na kupoteza moja na jana usiku ilicheza dhidi ya Olympiacos Piraes na kubakiza moja kujua hatma ya kucheza michuano hiyo na itacheza na AEK Mei 11.
Paok ilishinda dhidi ya AEK Athens 3-2, Olympiacos Piraes 2-1, Panathinaikos 2-1 na kupoteza Panathinaikos 2-1.
Olympiacos Piraes imeshajikatia tiketi ya kucheza michuano hiyo ikisubiriwa timu moja kati ya Panathinaikos, PAOK na AEK wanaowania nafasi ya pili.
Panathinaikos iko nafasi ya pili na pointi 56 tofauti ya pointi moja na PAOK ya tatu na pointi 55, huku AEK ikiwa na 53.