John Noble avunja ukimya ishu ya Fountain Gate

Muktasari:
- Hatua ya kipa huyo kuondoka kikosini imejiri baada ya makosa mawili aliyofanya katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga iliyopigwa Aprili 21, 2025, hali iliyosababisha kupelekwa kwenye kamati ya maadili ya klabu hiyo ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
KIPA wa Fountain Gate raia wa Nigeria, John Noble amevunja ukimya akithibitisha ni kweli kwa sasa ameondoka ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya kwenda kupumzika kwa wiki kadhaa, ingawa atarejea ili kujua hatima yake kama ataendelea kusalia au atavunja rasmi mkataba wake.
Hatua ya kipa huyo kuondoka kikosini imejiri baada ya makosa mawili aliyofanya katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga iliyopigwa Aprili 21, 2025, hali iliyosababisha kupelekwa kwenye kamati ya maadili ya klabu hiyo ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara, Noble aliruhusu bao la Clement Mzize katika dakika ya 38 baada ya kuutema mpira uliopigwa kichwa na Prince Dube aliyeunganisha frii-kiki iliyopigwa na Stephane Aziz KI.
Wakati Fountain ikijipanga kujipu mapigo, John Noble kwa mara ya pili tena alifanya makosa baada ya kushindwa kuumiliki mpira na kupiga pasi fupi iliyonaswa na kiungo mshambuliaji nyota, Stephane Aziz KI aliyepiga bao la pili katika dakika ya 43.
Baada ya bao hilo la pili, Noble akafanyiwa mabadiliko na benchi la ufundi chini ya kocha mkuu, Mkenya Robert Matano na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Parapanda, ambaye pia aliruhusu mabao mawili na mchezo huo kuisha kwa kichapo cha 4-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Noble alisema kwa sasa hayupo na timu hiyo kwa sababu ameenda kupumzika kutokana na presha kubwa aliyopitia, kisha baada ya hapo atarejea ili kujua hatima yake kama ataendelea kusalia kikosini humo au ataondoka.
"Nimeondoka ila sijavunja mkataba kama ambavyo wengi wao wanazungumza, uamuzi wa mwisho bado sijafanya ila ni kweli kwa sasa siko na timu na nimeondoka ili nipate muda wa kupumzika, itoshe kusema mimi ni mchezaji wa Fountain Gate," alisema.
Mwanaspoti linatambua mchezaji huyo anayemaliza mkataba wake mwisho mwa msimu huu, hataongezewa tena licha ya kuwapo kwa kipengele kinachomruhusu kuongezewa, huku ikielezwa viongozi hawana mpango wa kuendelea naye msimu ujao kikosini humo.
Hivi karibuni, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha aliliambia Mwanaspoti nyota huyo aliitwa kwenye kamati ya maadili, japo taarifa zinaeleza kikao hicho kilishindwa kufanyika kutokana na kutokuwepo kwa mchezaji husika.