Azam FC yashtukia kitu kwa Nizar

Muktasari:
- Ipo Hivi. Mara baada ya mechi ya fainali ya Kombe la Muungano, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Gombani na Yanga kubeba taji kwa kuifunga JKU kwa bao 1-0, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alionekana akizungumza na mchezaji huyo kwa muda mrefu uwanjani hapo.
WAKATI ikielezwa kuwa, Yanga iko katika mazungumzo na nyota wa JKU, Abubakar Nizar Othman, mabosi wa Azam FC wameweka wazi nyota huyo ni mali yao na hauzwi, hivyo wanaomtaka wasahau kuhusiana na hilo na mwishoni wa msimu huu watamrudisha.
Ipo Hivi. Mara baada ya mechi ya fainali ya Kombe la Muungano, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Gombani na Yanga kubeba taji kwa kuifunga JKU kwa bao 1-0, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alionekana akizungumza na mchezaji huyo kwa muda mrefu uwanjani hapo.
Nizar aliyecheza beki wa kulia, licha ya kuwa kwa asili ni kiungo mkabaji, aling'ara kutokana na kuwa mtulivu, makini na mwenye uwezo mkubwa wa kusoma mchezo. Mazungumzo yake na Hersi yaliibua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka waliokuwa uwanjani hapo.
Hersi alionekana akizungumza na kinda huyo akiwa sambamba na Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji. Tukio hilo liliibua hisia kuwa huenda Yanga imepania kumfuatilia kwa ukaribu kijana huyo ambaye pia alitangazwa kuwa Mchezaji Bora Chipukizi wa mashindano hayo.
Alipotafutwa, kuongelea nini kilitokea, Injinia Hersi alisema: "Ni mchezaji mzuri sana kwa umri wake. Ana kipaji cha asili na naamini kama ataendelea kuwa na nidhamu, anaweza kufika mbali. Pengine siku moja ataichezea Yanga."
Kwa upande wa Nizar alieleza furaha yake kwa kutambuliwa na viongozi wa Yanga. "Waliniambia hongera kwa kucheza vizuri na kwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi. Nimefarijika sana, inanipa hamasa kubwa ya kufanya zaidi," alisema kinda huyo mwenye miaka 16.
Nizar alianza soka akiwa na umri mdogo huko Zanzibar kabla ya kuwa sehemu ya akademi ya Azam ambako amenolewa na kocha Mohamed Badru na baadaye kujiunga na JKU kwa mkopo ili kupata nafasi zaidi ya kucheza mashindano makubwa.
Kombe la Muungano limekuwa jukwaa lake la kung'ara, na sasa jina lake linazungumzwa na wadau mbalimbali wa soka nchini. Wataalamu wa soka wanaamini kuwa iwapo atalelewa vizuri, Nizar anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji wa kizazi kipya watakaokuja kulitangaza taifa kimataifa.
Kwa sasa bado haijafahamika iwapo Yanga itachukua hatua rasmi za kuanza mazungumzo ya usajili, lakini kwa kauli ya Hersi na namna walivyomkaribia, kuna kila dalili kuwa jina la Nizar litatajwa kwenye mikakati ya baadaye ya mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat', amevunja ukimya na kuweka bayana klabu zinazomvizia mchezaji huyo zisahau kumpata kwa sasa kwani ni mali yao na kule JKU ameenda kucheza kwa mkopo tu.
Popat alisema ameona taarifa mbalimbali kwa baadhi ya vigogo wakimfuatilia kwa ukaribu, ingawa wanachopaswa kutambua mchezaji huyo ni mali yao na wala hauzwi.
"Nizar ni mchezaji halali wa Azam na sio JKU, kule tumempeleka kwa mkopo kwa sababu ya umri wake ili apate nafasi ya kucheza mara kwa mara, suala la timu nyingine kumnyemelea ni kutojua na mwisho wa msimu tutamrudisha," alisema Popat.
Popat alisema sio rahisi kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha Azam FC kutokana na wachezaji waliopo, ingawa wanachokifanya ni kumuandalia misingi bora wakiamini ni hazina bora ya baadaye na wanashukuru ameshaonyesha hilo.
"Tunaamini katika uwezo wake ndio maana tukaona tumpeleke JKU sehemu itakayokuwa nzuri kwake katika kukuza na kuendeleza kipaji chake, suala la yeye kucheza akirudi hilo litategemea benchi la ufundi, ila ni hazina yetu ya baadaye kikosini."