Sakho ampa Chama jezi yake namba 17

SIMBA jana walimtambulisha nyota wao wa kimataifa, Clatous Chama ambaye amerejesha kwenye klabu yake ya zamani huku Pape Sakho anayetumia jezi namba 17 iliyokuwa ikivaliwa na Mzambia huyo akisema yupo tayari kuiacha kiroho safi.

Kurejea kwa Chama ndani ya Simba kumewagusa Wanasimba wengi hivyo kumsubiri kwa hamu na atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokwenda Mbeya kucheza na Mbeya City.

Akizungumza na Mwanaspoti, Sakho alisema hajawahi kumuona Chama akicheza lakini amekuwa akisikia sifa zake hivyo anaamini ni mchezaji mzuri na kwamba hana tatizo na namba hiyo ya jezi iliyokuwa anaitumia kwani alipofika Simba hakuja na jezi.

“Sina tatizo na hii jezi kumwachia kwani sikuja Simba na hii jezi, nimemsikia Chama na ninaamini ni mchezaji mzuri ingawa sijawahi kumuona,” alisema Sakho ambaye anang’ara kwa sasa Msimbazi.

Habari kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa Sakho atapewa jezi namba 10 aliyokuwa akiitumia Ibrahim Ajibu ambaye amesajiliwa na Azam FC kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi mchezaji, Sakho aliibuka mchezaji bora wa jumla wa mashindano hayo huku pia akiwa amefunga mabao mawili sawa na aliyetangazwa Mfungaji Bora, Meddie Kagere anayekipiga naye Msimbazi.