Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo De Lima atishia kurudi uwanjani

Muktasari:

  • De Lima alikuwa akifanya maongezi na staa wa sasa wa Brazil, Neymar katika mahojiano maalumu yaliyoandaliwa baina ya mastaa hao wawili na alimtania Neymar kwamba wakati ulikuwa umefika kwa penalti za klabu hiyo kupigwa na Rais wa klabu hiyo ambaye ni yeye mwenyewe.

RIO DE JANEIRO,BRAZIL.STAA wa zamani wa Timu ya Taifa ya Brazil, Ronaldo de Lima ametania kuachana na suala la kustaafu soka na kurudi uwanjani baada ya kushuhudia timu yake anayoimiliki Real Valladolid ikikosa penalti kadhaa msimu huu.

De Lima ambaye alitwaa Kombe la Dunia na Brazil kule Japan mwaka 2002 amekuwa mmliki mkubwa wa klabu hiyo tangu Septemba 2018 baada ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu hiyo kwa dau la Pauni 26 milioni.

Valladolid inashika nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania na De Lima ameonyesha kuchoshwa na kitendo cha wachezaji wake wa timu yake kukosa penalti kadhaa walizopewa na waamuzi msimu huu wakati huu timu hiyo ikipambana isishuke daraja.

De Lima alikuwa akifanya maongezi na staa wa sasa wa Brazil, Neymar katika mahojiano maalumu yaliyoandaliwa baina ya mastaa hao wawili na alimtania Neymar kwamba wakati ulikuwa umefika kwa penalti za klabu hiyo kupigwa na Rais wa klabu hiyo ambaye ni yeye mwenyewe.

“Penalti muhimu kwa sasa inabidi zipigwe na Rais wa klabu. Kwa sasa mimi ni Rais wa klabu. Mwaka huu tumepewa penalti tano. Tumezikosa zote hapa Valladolid. Najiandaa kurudi uwanjani mwenyewe. Penalti zinapigwa vibaya. Ni jukumu kubwa sana.” alisema Ronaldo.

Ronaldo anaamini kwamba ni suala la muda tu kabla ya Neymar hajaipita rekodi yake ya ufungaji ya muda wote katika kikosi cha timu ya taifa. Lakini pia kuna uwezekano mkubwa akaipita rekodi ya mfalme wa kandanda duniani, Pele.

Pele anaongoza kwa kufunga mabao katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil akiwa na mabao 77 baada ya mechi 92 huku De Lima akifuatia na mabao 62 lakini Neymar mpaka sasa ana mabao 60 na katika umri wa miaka 27 anatazamiwa kumpiku De Lima na kisha Pele.

“Unakwenda kunipiku katika ufungaji wa mabao timu ya taifa. Nasubiri kwa hamu. Ni suala la muda tu. Nenda nipite na niache na mabao yangu. Wewe bado mdogo. Una mambo mengi ya kupata,” alisema Ronaldo akimwambia Neymar.

Ronaldo ambaye pia alitwaa Kombe la Dunia na Brazil mwaka 1994 nchini Marekani ingawa hakugusa mechi yoyote anakiri kwamba ni kitu cha kawaida kwa mastaa wenye majina makubwa kutaniwa zaidi katika kambi ya timu ya taifa ya Brazil.

“Nilitaniwa sana pia. Ulikuwa utani mbaya. Ilikuwa ni sehemu ya utamaduni wetu, au sio? Wakubwa pia waliwatania watoto ‘Osha viatu vyangu’. Kuichezea timu ya taifa ya Brazil ni ndoto za kila mtoto. Tulikuwa huku tukitazama Kombe la Dunia, hii pia ilizalisha upendo tuliokuwa nao katika soka.”

“Kuichezea timu ya taifa ni njia pekee ya kuionyesha nchi yangu mapenzi na heshima. Unaota ndoto za kuwa mwanasoka na unapenda sana soka. Ghafla unakuwa shujaa wa malaki ya watoto. Inashangaza sana.” alisema De Lima.

Kwa sasa Ronaldo ni mmoja kati ya washambuliaji hatari kuwahi kutokea duniani amekuwa Mfanyabiashara mkubwa kutokana na kukusanya pesa nyingi wakati akicheza soka na aliuziwa klabu hiyo ya Valladolid ya La Liga huku yeye mwenyewe akiwa na uzoefu wa kucheza La Liga ambako aliwahi kutamba na klabu za Barcelona na Real Madrid.

Alikabidhiwa timu hiyo ya Valladolid, mji uliopo Kaskazini Magharibi mwa Hispania akiwa kando ya Rais wa zamani wa Valladolid, Carlos Suarez na Meya wa jiji hilo, Oscar Puente. Rais Suarez alidai kwamba kumuuzia hisa Ronaldo ilikuwa njia pekee kwa klabu hiyo kufanikiwa.

Naye Ronaldo alidai kwamba anatazamiwa kuijenga Valladolid kuwa moja kati ya timu bora na kushindania mataji La Liga sambamba na klabu nyingine kubwa za Hispania kama vile Barcelona, Real Madrid, Valencia, Atletico Madrid na wengineo.

“Nimepitia katika hatua nyingi za mazoezi katika soka kwa ajili ya kujiandaa. Soka ni mchezo ninaoupenda. Utawala wangu katika soka utajitambulisha kwa mambo haya ya ushindani, uwazi, mapinduzi na kuwa karibu na jamii,” Alisema Ronaldo alipoinunua timu hiyo mwaka jana.

Kabla ya Ronaldo kuinunua timu hiyo, ilikuwa daraja la kwanza na uvumi wa kuuzwa kwa klabu hiyo ulikuja tangu Mei mwaka jana lakini ikasubiriwa mpaka Juni kama timu hiyo ingepanda daraja. Ilipopanda daraja ndipo Ronaldo alipopata nafasi ya kuinunua.

Wamiliki kutoka China na Amerika waliripotiwa kutaka kuinunua timu hiyo lakini Rais wa zamani Suarez alidai kwamba waliona ofa ya Ronaldo ni nzuri zaidi na inavutia. Valladolid ilimaliza nafasi ya tano msimu wa 2017-2018 kabla ya kucheza mechi za mtoano na kupanda Ligi Kuu lakini Ronaldo asipoongeza juhudi wanaweza kurudi walikotoka.