Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Riadha imetafunwa namna hii-1

Juma Ikanga wa Tanzania katika mbio za kimataifa

Muktasari:

Wanariadhaa kama Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa na wengine ni kati ya wakimbiaji wa Tanzania walioitangaza vyema Tanzania kwa mafanikio waliyopata katika mashindano mbalimbali. Miaka ya 1980-1990 Tanzania ilitisha kwenye riadha kuanzia mbio ndefu, mpaka zile fupi kwa wanariadhaa wake kung’ara kila walipoiwakilisha nchi.

ZAIDI ya miaka 30 iliyopita Tanzania ilitia fora na kung’ara kwenye mchezo wa riadha. Wakimbiaji wake mbalimbali walijizolea sifa kemkem Afrika na duniani kutokana na jinsi walivyokuwa wakishinda karibu kila shindano na kutwaa medali tofauti.

Wanariadhaa kama Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa na wengine ni kati ya wakimbiaji wa Tanzania walioitangaza vyema Tanzania kwa mafanikio waliyopata katika mashindano mbalimbali. Miaka ya 1980-1990 Tanzania ilitisha kwenye riadha kuanzia mbio ndefu, mpaka zile fupi kwa wanariadhaa wake kung’ara kila walipoiwakilisha nchi.

Hata hivyo, hali imekuwa tofauti kwa miaka ya karibuni, mchezo huo umedorora na hata wakimbiaji wake hawatambi tena kimataifa, wamefunikwa kabisa na wenzao kutoka nchi za Ethiopia, Kenya na hata Burundi. Kipi kilichoukumba mchezo huo?

Mwanaspoti limezungumza na baadhi ya nyota hao wa zamani na viongozi wenye dhima ya mchezo huo na wamedokeza sababu ya kifo cha mchezo huo wa riadha.

Kuporomoka

Bayi anasema sababu ya mchezo wa riadha kupoteza mvuto nchini Tanzania ni kusimamishwa kwa michezo shuleni. Jambo lililotokea mwaka 1996 chini ya uongozi wa aliyekuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai.

Anasema hapo zamani hata sasa timu mbalimbali kama za watu binafsi, majeshi, zinatafuta vijana wadogo tangu miaka minane na kuendelea kutoka shuleni, ikiwatunza na baadaye wanakuja kuwa wanamichezo wazuri.

Hata hivyo, baada ya kusimamishwa kwa mpango huo, njia nyingine ya kugundua vipaji hivyo ikawa hakuna na hapo ndipo Tanzania ikaporomoka.

Kenya

Bayi akaenda mbali na kutolea mfano nchi ya Kenya, anasema imepata umaarufu kupitia mchezo huo kwa sababu waligundua mapema, wakawekeza shuleni na sasa wanavuna walichopanda kutokana na kufanya kwao vizuri.

“Kufungwa kwa michezo shuleni ndiyo sababu ya riadha kupotea nchini mwetu, kwa kawaida kipaji cha mwanamichezo utakigundua tangu utotoni, baada ya hapo, waliokuwa wanaibuka ni wale wa ukubwani,” anasema Bayi.

“Mwanariadha anaibuka kwa sababu anapenda riadha na anajua kukimbia, lakini mafunzo hana. Wanariadha waliopo sasa ni wale waliojiendeleza wenyewe kizazi ambacho kinaishia kwa sasa.

“Kwa kawaida riadha ni lazima mtu afundishwe na kulelewa katika mazingira hayo hadi ukubwani, hapo ndipo utegemee mwanariadha mzuri. Lakini kwa hawa wa kipindi hiki ni ngumu kupata kile tunachokihitaji kwa sababu sehemu kubwa zinakuwa ni juhudi za mhusika mwenyewe lakini zile mbinu haswa za riadha anakuwa hana.

“Umeona tangu michezo hiyo isimamishwe shuleni hadi sasa ni kama miaka minane, kile kizazi kilipoishia miaka ile kikapotea kikaja hicho ambacho kinalalamikiwa, ambacho hakina maelezo yoyote ya mchezo huo.

“Hata hivyo, tangu utaratibu huu urudi shuleni nina uhakika miaka michache ijayo tutakuwa na wanaridha wazuri ambao tuliwalea shuleni na Watanzania watafurahi.

Samson

Mwanariadha mwengine aliyewahi kuiletea Tanzania heshima. Samson Ramadhani kwa upande wake anasema maandalizi ya zima moto ni tatizo la wakimbiaji wengi wa Tanzania ambao hupewa dhamana ya kuiwakilisha nchi.

“Kila unachotaka kiwe na mafanikio, lazima ukiandae kwa muda mrefu, wakimbiaji wengi huandaliwa kwa wiki mbili au moja wanapokwenda kwenye michuano ya kimataifa jambo ambalo haliwezekani kututoa hapa tulipo na kutufikisha hatua nyingine nzuri.

“Tanzania ina vijana wengi ambao wana uwezo mkubwa wa kuandaliwa na kuwa bora kama miaka ya nyuma walipokuwa wanakimbia kina Bayi au sisi, tuliandaliwa kwa miaka mingi mpaka kufikia hatua ya kukimbia kimataifa,” anasema na kuongeza;

“Lakini kwa sasa wanariadha wanaokotwa tu na kupelekwa kwenye mashindano hapo ni lazima tufeli tu,” anasema.

Mwanaridha huyo anasema anakumbuka aliandaliwa kwa muda wa miaka kama 10 kabla ya kuja kutamba anga za kimataifa.

“Binafsi niliandaliwa kwa muda mrefu tangu nipo shule ya msingi mwaka 1993 na nimeanza kukimbia mashindano ya kimataifa mwaka 2003, nilichukua muda mrefu, huo muda unatosha sana kwa mchezaji kuiva kushiriki mashindano yoyote kwa upinzani.”

Mabonanza

Samson anasema sasa riadha imegeuzwa kama mchezo wa mabonanza ambayo waratibu wake wakijisikia kupiga pesa kwa wadhamini wanaandaa shindano lake kisha mambo yakaishia hapo.

“Kipindi hiki hakuna wanariadha wenye ushindani, wengi wanatokea kwenye mabonanza hivyo wanakuwepo kwa ajili ya masilahi yao na si masilahi ya nchi kama ilivyokuwa zamani, hata akiwekwa kambini anaona kama mtumwa tu, akili yake haipo kwa ajili ya kulitetea taifa.”

Itaendelea kesho Ijumaa