PAOK, Southampton zamtaka Samatta

Muktasari:
- Nyota huyo wa zamani wa Aston Villa kwa sasa yuko nchini kwa mapumziko baada ya Ligi ya Ugiriki kutamatika wikiendi iliyopita na chama lake kumaliza katika nafasi ya nne likifuzu michuano ya Europa League.
MKATABA wa mshambuliaji wa PAOK, Mbwana Samatta unatamatika mwishoni mwa mwezi huu na inaelezwa timu hiyo tayari imeanza mazungumzo ya kumuongezea kuendelea kusalia kikosini hapo.
Nyota huyo wa zamani wa Aston Villa kwa sasa yuko nchini kwa mapumziko baada ya Ligi ya Ugiriki kutamatika wikiendi iliyopita na chama lake kumaliza katika nafasi ya nne likifuzu michuano ya Europa League.
Sasa inaelezwa viongozi wa timu hiyo wameanza mazungumzo na nyota huyo aliyeweka rekodi mbalimbali Ulaya.
Chanzo kiliambia Mwanaspoti kuwa mbali na PAOK ambao wanapambana kumbakisha kutokana na kile alichokionyesha mwishoni, Southampton imevutiwa na huduma yake.
Ikumbukwe Southampton hivi karibuni pia iliwahi kumuulizia Mtanzania, Novatus Miroshi anayekipiga Goztepe ya Uturuki.
“Ninachofahamu ofa ziko nyingi nje ya hizo nilizokutajia kuna nchi nyingine kama mbili hivi na PAOK walikuwa kwenye mpango wa kumuacha lakini baada ya kurejea alipokuwa anauguza majeraha wakabadilisha uamuzi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Kwa sasa anasikilizia ofa ipi itakuwa nzuri kama ni PAOK au Southampton, uamuzi wake wa mwisho ni kwenye mkwanja mrefu tu ila kokote anacheza.
“Southampton ilimtafuta kitambo kidogo wakati ule kabla haijashuka daraja, huko nako pia anasikilizia.”
Samatta msimu huu amemaliza na mabao manne na asisti moja Ligi Kuu.