Rhino, Mbao FC uwanjani

Dar es Salaam. Michezo ya kwanza ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inamalizika leo kwa Rhino Rangers kucheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Hadi sasa timu zilizoshuka daraja zimeonekana kuanza ligi kwa kusuasua huku Lipuli pekee akiondoka na pointi tatu baada ya kuifunga Mawenzi Market mabao 2-1 mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro juzi Jumamosi.

Wakati Lipuli ikiondoka na ushindi huo, Singida United ilichezea kichapo cha mabao 2-0 mbele ya Geita Gold mchezo uliofanyika Uwanja wa Nyankumbu, Geita.

Mabao hayo yalifungwa na Venance Ludovick dakika ya 19 na 34 na kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili huku Fountain Gate ikiwa kileleni mwa msimamo baada ya kuichapa 3-0 Allince FC.

Katika michezo ya ufunguzi wa FDL iliishuhudia Ndanda iliyoshuka daraja nayo ikibanwa mbavu ya bao 1-1 na African Lyon katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ushindi huo wa Geita inayoongozwa na Kocha Fredy Felix ‘Minziro’ umekuwa mwendelezo mzuri wa msimu uliopita baada ya kufanikiwa kumaliza nafasi ya pili na kuishia hatua ya mtoano.

Matokeo mengine Pamba FC iliifunga 2-1 Arusha FC, Njombe Mji ikilala 1-0 dhidi ya Mbeya Kwanza na Gipco FC ikichapwa 1-0 na Boma FC na Majimaji ikilala 2-1 kwa African Sports.

Kitayosce FC inayonolewa na Idd Cheche ikiwa nyumbani Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ililala kwa bao 1-0 dhidi ya Transit Camp.

Kocha wa AFC, Atuga Manyundo aliwatupia lawama waamuzi wa mchezo huo kuwa sababu ya kupoteza kwao kutokana na kuendelea kuchezesha wakati dakika 90 zikiwa zimemaliza.

“Watu wanafanya kama wamepewa maelekezo au wametumwa,” alisema.