Refa Simba, Yanga hana baya

Tuesday May 04 2021
mwandembwa pic
By Charles Abel

Mzani wa refa, Emmanuel Mwandembwa atakayechezesha mechi ya Simba na Yanga, Jumamosi Mei 8, 2021 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa umebalansi kutokana na uwiano mzuri wa matokeo ya mechi za timu hizo ambazo amechezesha msimu huu.

Takwimu za Ligi Kuu msimu huu zinaonyesha timu hizo mbili zimepata matokeo yanayoshabihiana katika michezo ya Ligi Kuu ambayo zimechezeshwa na Mwandembwa kutokea mkoani Arusha.

Takwimu zinaaonyesha refa huyo msimu huu amekuwa na bahati kwa timu hizo zote kwani katika jumla ya mechi saba ambazo amezichezesha Yanga na Simba katika Ligi Kuu, hazijawahi kupoteza mchezo.

Mwandembwa msimu huu, amechezesha mechi nne za Yanga ambapo kati ya hizo, imeibuka na ushindi mara tatu na kutoka sare katika mchezo mmoja, ikifunga jumla ya mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu.

Mechi ya kwanza kwa Mwandembwa kuichezesha Yanga msimu huu ilikuwa ni ile ya kwanza katika ligi dhidi ya Prisons iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 6, 2020 iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, kisha akachezesha mechi ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Azam, Novemba 25, 2020.

Februari 20 mwaka huu, alichezesha mechi ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na mechi nyingine aliyoichezesha ni ile ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Biashara United, Aprili 17 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Advertisement

Kwa upande wa Simba, refa huyo amechezesha jumla ya mechi tatu za Ligi Kuu msimu huu ambapo kati ya hizo wameshinda mechi mbili na kutoka sare moja, wakifunga mabao matano huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.

Alichezesha mechi ambayo Simba ilishinda kwa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, Februari 4 na ya pili ilikuwa ni ile ambayo ilitoka sare ya bao 1-1 na Prisons, Machi 10 mwaka huu.

Aprili 24 mwaka huu, refa huyo alichezesha mechi ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.Advertisement