Ramani ya ushindi Simba ilikuwa hivi...

Sunday November 28 2021
Ramani PIC

Mvutano wa wachezaji wa Simba dhidi ya Red Arrows baada ya bao la Bernad Morrison. Picha| Loveness Bernad

By Daudi Elibahati
By Damian Masyenene

WANACHAMA wa Simba wameipa mchongo timu yao kuibuka na ushindi katika mchezo wao wa leo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows katika Uwanja wa Mkapa.

Timu hizo zinakutana hatua ya mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi na baada ya mchezo wa leo, wa marudiano utapigwa Zambia Desemba 5.

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Aden Rage alisema Simba inapaswa kuuchukulia mchezo huo kwa umakini mkubwa na kuepuka kilichowatokea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy.

“Naamini viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wamejifunza kutokana na makosa yaliyopita, hivyo wanapaswa kutambua wana dakika 180, za jasho na damu kwa mashabiki wao ili kuwasahaulisha yaliyotokea huko nyuma,” alisema Rage.

Mwenyekiti mwingine wa zamani wa timu hiyo, Swedy Mkwabi alisema licha ya wapinzani wao kuwa nafasi ya sita kwenye ligi ya Zambia ila hawapaswi kuwadharau bali wanatakiwa kuwa makini kwa sababu Red Arrows wanacheza kwa ushirikiano mkubwa.

“Ushindi wa nyumbani utatoa taswira halisi kuelekea mechi ya marudiano hivyo jukumu pekee lililobaki ni la wachezaji kujituma mara mbili zaidi ili kuwapa raha mashabiki zao,” alisema.

Advertisement

Kwa upande wa beki wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa aliongeza; “Baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa kila kitu kilibadilika hii ina maana walitambua wapi walikosea naona kabisa wakishinda kwa sababu ya morali waliyokuwa nayo ingawa sio mchezo mwepesi kwa kuwa kila timu iliyoko huku sio ya kubeza,”

Beki wa zamani wa Yanga, Ladislaus Mbogo naye alikuwa na haya; “Simba wamefanya usajili mzuri tatizo lililowapata kwa Jwaneng waliteleza tu shida yetu tunataka vitu vya haraka, wachezaji wafanye kazi kubwa nyumbani wapate mabao mengi wajiamini tu wanaweza.

“Wana timu bora wanaweza kufanya vizuri zaidi wapambane wasidharau bali wacheze kama wanacheza na Al Ahly, wajitoe kwa moyo wote wapate ushindi mkubwa nyumbani, wasiingie na presha ya mashabiki huo ni mchezo muhimu,” alisema.

Kocha wa TSC Queens ya Mwanza, Hawa Bajanguo alisema Simba inatakiwa kuingia kwenye mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani na kuuchukulia mchezo kama fainali kwao.

“Wanatakiwa waiheshimu timu pinzani kocha atakuwa ameona mapungufu na kuwaweka vizuri wachezaji kisaikolojia na mbinu naamini atakayepangwa atafanya vizuri,” alisema Hawa.

Advertisement