Kwa Simba hii Arrows wataomba poo

Kwa Simba hii wataomba poo Red Arrows

DAKIKA 45, za kipindi cha kwanza zimemalizika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji Simba kuongoza mabao 2-0 dhidi ya Red Arrows katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu zote zilianza kwa kushambuliana kwa zamu huku tatizo pekee likiwa ni maji yaliyopo kwenye Uwanja huo kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika Jiji la Dar es Salaam.

Changamoto hiyo ilibidi Simba kutumia Mipira mirefu ambayo ilileta tija baada ya Bernard Morrison kuiandikia Simba bao la Utangulizi dakika ya 15, akipiga faulo iliyomshinda kipa Charles Kalumba.

Wakati Red Arrows wakiendelea kutafakari juu ya kusawazisha bao hilo alikuwa ni mshambuliaji Meddie Kagere aliyepachika bao la pili dakika ya 18, ya mchezo baada ya kazi zuri iliyofanywa na Bernard Morrison.

Dakika ya 30, Simba ilikosa mkwaju wa penalti kupitia kwa Bernard Morrison baada ya kipa wa Red Arrows Charles Kalumba kupangua na kuisaidia timu yake kuepuka kufungwa bao la tatu.

Licha ya mabadiliko kwenye kikosi cha leo cha Simba tofauti na kile kilichocheza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting ila wachezaji wote walionyesha kujituma na kufanikiwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani katika dakika hizi 45, za kwanza.

Matokeo haya yanakuwa ya faida kwa Simba huku Red Arrows wakiwa na mtihani mgumu wa kusawazisha mabao hayo kipindi cha pili.