Duh! Simba mafia sana

PICHA NA LOVENESS BERNARD

KUONDOLEWA katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni jambo lililowakera mno mabosi wa Simba na sasa wamekubaliana kwa kauli moja kwamba liwalo na liwe lazima Red Arrows wapigwe Jijini Dar es Salaam kesho. Mwanaspoti linafahamu Jumatano asubuhi ya wiki hii mabosi wanne wa ngazi ya juu Simba walijifungia kwenye jumba la kifahari la tajiri mmoja kati yao wakiwa pamoja na makocha wao watatu, Pablo Franco sambamba na wasaidizi wake, Selemani Matola na Hitimana Thiery na hapo ndipo mechi ya kesho Jumapili ilipochezeka na kumalizwa hata kabla Arrows hawajatua.

Inaelezwa kikao hicho kilitumia saa 1:30, kiliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’, Mtendaji mkuu, Barbara Gonzalez, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu pamoja na Mwenyekiti kamati ya usajili Kassim Dewji.

Kwenye kikao hicho, Pablo na wasaidizi wake walieleza sababu ambazo zilichangia kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na mipango, mbinu wanazozifanya wakati huu katika mazoezi ili kila mchezaji kutambua umuhimu wa mechi hiyo na wale watakaopata nafasi ya kucheza wakaonyeshe viwango bora.

Baada ya hapo benchi hilo la ufundi liliomba mshikamano uendelee kuzidi kati yao si katika mchezo huo wa mzunguko wa kwanza bali hata ule wa marudiano pamoja na mingineyo iliyokuwa mbele yao kwani wote lengo lao ni moja kuhakikisha Simba inafanya vizuri na kuchukua mataji.

Benchi la ufundi baada ya kumaliza ya upande wao, viongozi kila mmoja alieleza umuhimu wa kupata matokeo mazuri dhidi ya Red Arrows na jinsi walivyojipanga kihamasa.

Viongozi hao walimueleza Pablo afanye majukumu yake ya kiufundi vizuri na kuwapatia kila mbinu wachezaji kuhakikisha si kuwafunga Red Arrows bila kushinda katika mechi nyingine nyingi lakini aliambiwa kutakuwa na bonasi za pesa kama watashinda na huo ndio utaratibu wa klabu ulivyo.


KAULI YA UONGOZI

Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi, Asha Baraka alisema wao kama uongozi wanafahamu majukumu yao na tayari wameyafanya na wanaendelea kuyafanya cha msingi ni kila Mtanzania kuisapoti Simba kwa kuwa ndio wawakilishi pekee kwa sasa.

“Sisi kama uongozi tuko imara sana, naongea kama mwanasimba na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, tumejiandaa kwa kila kitu kama uongozi kila mtu anafanya majukumu yake wachezaji nao watumie vizuri dakika 90, bodi tunawekeza kwenye mpira na sio maneno ni vitendo tu tunauhakika tutafanya vizuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani.”alisema Asha. Kocha wa Simba, Pablo aliliambia Mwanaspoti kwamba wameiandaa timu kisaikolojia na ana imani kwamba moto waliouwasha kwenye mechi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Ligi hautazimika.

Aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Habari ya Simba, Ezekiel Kamwaga ambaye kwa sasa yuko masomoni nchini Uingereza aliiambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kuwa anaimani na kikosi chake kuelekea mchezo huo.

Simba imepania kufuzu na kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya mipango yao ya awali ya kucheza hatua hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika kufeli mapema. Simba ikishinda mechi mbili ile ya kesho nyumbani na ugenini watafuzu makundi ya Shirikisho.