Punguzo la bei Kilimanjaro Marathon mwisho kesho

Monday January 13 2020
Kilimarapic

Dar es Salaam. Waandaji wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon wamesema mwisho wa punguzo la bei kwa wanaoshiriki mbio za kilometa 42 na 21 litakwisha kesho Januari 14, 2020.

Mbio za Kilimanjaro Marathon zimebakiza mwezi mmoja na nusu kabla ya kufanyika hivyo waandaaji wamesema usajili uliokuwa ukiendelea kwa njia ya mtandao na Tigopesa na kuwataka washiriki waendelee kujisajili leo na kesho kwa wingi kabla ya saa sita usiku ili kupata punguzo hili la asilimia 20.

“Mtu atayejiandikisha sasa bei ni 15,000 kwa mbio za kilomita 42 na 21 na elfu tano kwa mbio za kilomita 5 maarufu kama fun run. Baada ya Jumane itakuwa Sh 20,000. Hii ni kwa watanzania na raia wa nchi za Afrika Mashariki tu.

Washiriki wanajisajili kwa kupitia www.kilimanjaromarathon.com na kwa Tigopesa kwa kubonyeza *149*20#.

 Mkurugenzi wa Mbio hizo nchini, John Bayo alisema usajili utafungwa Februari 16, 2020 au pale idadi maalumu ya washiriki inayotakiwa kwa mbio zote tatu (Kilimanjaro Premium Lager Km 42, Tigo km 21 na Grand Malt Km 5) ikifikiwa ili kuhakikisha kuwa mbio hizo zinaendana na viwango vya Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) ili kuhakikisha usalama unazingatiwa.

Kwa mujibu wa Bayo hii pia itahakikisha washiriki wanafurahia mbio hizo bila ya msongamano na pia kutoa nafasi kwa waandaaji waweze kutoa huduma zinazotakiwa katika njia ya mashindano na sehemu ya kumalizia pia.

Advertisement

Kwa wageni wakazi au wenye vibali vya kuishi na kufanya kazi na wale wa nchi za SADC watalipa USD 35 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5 kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020 lakini kuanzia Januari 15, 2020 hadi Februari 16, 2020 wanaojisajili watalipa USD 45 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5.

Washiriki wa kimataifa watalipa USD 70 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5 kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020 na kuanzia Januari 15 hadi Februari 16, 2020 watalipa USD 85 kwa km 42 na Km 21 na USD 5 kwa km 5.

Washiriki wamekumbushwa kuhusu vituo vya kuchukulia namba zao za ushiriki kwa Dar es Salaam ni Mlimani City kuanzia February 22-23, 2020, Arusha ni Hoteli ya Kibo Palace kuanzia Februari 25-26 na Moshi ni Hoteli ya Keys kuanzia Februari 27-28.

“Washiriki watatakiwa kujitambulisha na kuthibitisha kuwa wameshalipia kabla ya kukabidhiwa namba zao,” ilisema taarifa ya waandaaji.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema muamko ni mkubwa na wanategemea kuwa mbio za mwaka huu zitafana zaidi na kuwataka Watanzania waendelee kufanya mazoezi ili kujihakikishia nafasi nzuri na zawadi zibaki nyumbani.

Kilimanjaro Premium Lager imekuwa imdhamini mkuu wa mbio hizi tangu kuanzishwa kwake miaka 18 iliyopita.

Naye Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema usajili kwa kupitia Tigo Pesa umepata muamko mkubwa kwani kwa sasa hakuna usajili wa makaratasi.

Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2020 ni Kilimanjaro Premium lager, Tigo, Grand Malt Kilimanjaro Water, TPC Limited, Simba Cement, Barclays Bank na watoa huduma rasmi ni Kibo Palace Hotel, Keys Hotel, GardaWorld Security, Precision Air na CMC Automobiles.

Mashindano ya Kilimanjaro Marathon yanayoandaliwa na Wild Frontiers na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions, yanatarajiwa kufanyika Machi 1, 2020 katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Advertisement