Promota wa Mwakinyo afunguka

PROMOTA Benjamin Shalom aliyeandaa pambano la Hassan Mwakinyo na Liam Smith amevunja ukimya wa pambano la marudiano ikiwa ni siku kadhaa tangu bodi ya kusimamia ngumi ya Uingereza (BBBC) kumfungia Mtanzania huyo kuzichapa nchini humo.

Wiki iliyopita, mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) ulibainisha bondia huyo namba moja nchini amefungiwa kupigana nchini humo kwa muda usiojulikana kabla ya Mwakinyo kueleza amepewa siku 45 kwa mujibu wa kanuni za ngumi nchini humo.

Baada ya kupigwa kwa TKO ya raundi ya nne na Smith Septemba 3, Shalon alieleza kuwa watarudiana tena Januari mwakani, lakini alidai kutofahamu kilichosababisha Mwakinyo kutoendelea na pambano lililopita.

“Nilipoona pambano limesimama nilishangaa, nikamuuliza refa kuna nini? Alisema hakuona kitu chochote na yeye hakuelewa kwanini huyu mtu ameacha pambano. Hata refai alishangaa, alimuona jamaa (Mwakinyo) yuko kwenye control ya mchezo, lakini ghafla tu ameshindwa kuendelea, hivyo alichukulia kama kajiangusha.

“Ila Mwakinyo ni bondia hatari. Tunamfahamu na amewahi kufanya maajabu hapahapa Uingereza na ana rekodi nzuri, hivyo sina hakika sana kama alijiangusha au vinginevyo,” alisema promota huyo.

Mwakinyo baada ya pambano hilo alidai kwamba alipatwa na maumivu ya kifundo cha mguu ambayo yalisababisha kuacha pambano na kuruhusu kipigo cha TKO, licha ya kwamba alikuwa akiongoza baadhi ya raundi.