Prisons yawachezesha kwata Ihefu

Wednesday September 15 2021
kwata pic
By Saddam Sadick

Kyela. Mashindano ya 'Mbeya Pre season' yanaendelea kushika kasi kwenye uwanja wa Mwakangale wilayani hapa, huku Prisons ikianza vyema kwa kuichakaza Ihefu bao 1-0.

Mchezo huo ambao ulikuwa wa kundi B, timu zote zilishuka dimbani kwa ari na morari ambapo, Ihefu waliingia kwa kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 walioupata katika mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Ken Gold.

Katika mchezo wa leo Jumatano, makocha wa timu zote waliweka nyota wao wote ili kuona ubora na udhaifu wao na mashabiki kufurahia burudani ndani ya uwanja kutokana na wachezaji kuonesha kandanda safi.

Ramadhan Ntobi ndiye alikuwa shujaa katika mpambano huo baada ya kufunga bao pekee katika dakika ya 47 lililoipa pointi tatu muhimu Prisons.

Ihefu walipambana kisawazisha bao hilo, lakini ngome ya 'Wajelajela' hao ilikuwa imara zaidi kuhakikisha inadhibiti hatari zote hadi dakika 90 zinamalizika.

Kocha wa Ihefu, Zuberi Katwila amesema pamoja na kwamba walihitaji ushindi lakini anafurahia muunganiko kwa vijana wake kwani mechi ya kwanza kikosi kilichotumika ni tofauti na leo.

Advertisement

"Naamini tutakuwa sawa hadi mashindano haya yanamalizika, kimsingi nafurahi muunganiko kwa sababu mechi iliyopita nilitumia sura tofauti na za leo" amesema Katwila.

Kocha wa Prisons, Salum Mayanga amesema atatumia michuano hii kusahihisha mapungufu yaliyoonekana msimu uliopita.

"Hususani safu ya ushambuliaji ilikuwa tatizo kubwa kwangu msimu uliopita, hivyo kwa sasa nalitazama sana ili lisijirudie" amesema Mayanga.

Advertisement