Prisons bado wapo sana Ligi Kuu

Mbeya. Ilikuwa mechi ya jasho. Ndivyo unaweza kuelezea kufuatia mpambano mkali uliowakutanisha JKT Tanzania dhidi ya Tanzania Prisons, huku Tanzania Prisons ikifanikiwa kubaki Ligi Kuu msimu ujao.
Mpambano huo uligubikwa na matukio mengi ndani na nje ya uwanja kila timu ilihitaji ushindi ili kucheza Ligi Kuu msimu ujao na wenyeji kujihakikishia nafasi hiyo kwa mabao 2-1.
Katika mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa, JKT Tanzania walitangulia kupata bao la kuongoza dakika ya 35 kupitia kwa Straika na kinara wa mabao kikosini humo, Edward Songo baada ya beki wa Prisons, Doto Shaban kuonekana akiugusa mpira kwa mkono eneo la hatari.
Hata hivyo kabla ya kupatikana bao hilo, mabeki wa Prisons wakiongozwa na Jumanne Elfadhir walifanya kazi nzuri ya kuokoa hatari nyingi zilizokuwa zikielekea langoni mwao.
Bao hilo lilionekana kuwachanganya Prisons na kupaniki huku wakijaribu kushambulia lakini walikutana na ugumu kwa wapinzani na kufanya kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao hilo.
Wakati mwamuzi, Ramadhan Kayoko akimaliza dakika 45 za kwanza, benchi la ufundi la Prisons liliwafuata waamuzi hao wakionekana kuwatupia lawama kwa uamuzi hao.
Kama haitoshi wakati wachezaji wakiingia vyumbani, manusura zipigwe ngumi kati ya Maafande wa JKT Tanzania na Prisons, ambapo wenyeji walizuia wachezaji wa JKT kutotumia mlango wa kuingilia wakitaka wapite upande wao, hali iliyowaamsha 'Wajeda' hao na kuwasukuma mbali Wajelajela.
Kipindi cha pili kilianza kwa Wajelajela kufanya mabadiliko kwa kumtoa Oscar Paul na kuingia Benjamin Asukile, huku wapinzani wakimpumzisha Omary Ramadhan na kuingia Daniel Mecha.
Prisons ilipambana na dakika ya 69 Asukile aliisawazishia bao timu yake na kuamsha shangwe kwa mashabiki ambao walikuwa wamepoa kwa muda mrefu lakini akiongeza ari na morari kwa wenzake uwanjani.
Dakika ya 80 manusura JKT Tanzania wapate bao lakini uimara wa Kipa wa Prisons, Edward Mwakyusa kupangua mashuti mawili ya papo kwa papo na kuwaacha wadau wa soka na mshangao.
Mchezo huo haukuisha salama kutokana na rafu za hapa na pale, lakini ilishuhudiwa ngumi kwa wachezaji katika dakika za nyongeza iliyomfanya Kayoko kutembeza kadi nyekundu kwa Elfadhir na Asukile wote wa Prisons.