Phiri akubali yaishe kwa Mayele Ligi Kuu

KASI ya Fiston Mayele imemuibua kinara wa upachikaji wa mabao Simba, Moses Phiri aliyekiri kuwa majeraha yamemuondoa kwenye ushindani, huku akiwataja John Bocco na Said Ntibazonkiza kuwa wanamuongezea presha Mkongoman huyo wa Yanga.

Phiri, aliyepo nje ya uwanja kwa wiki mbili sasa baada ya kuumia kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar ameshaanza mazoezi mepesi tayari kwa kurejea uwanjani huku akiwa na mabao 10 aliyofunga katika mechi 15 za duru la kwanza, matano nyuma na aliyonayo Mayele.

Akizungumza na Mwanaspoti, Phiri alisema ushindani kwenye ufungaji unazidi kuwa mkubwa kasi yake imesimama kutokana na kusumbuliwa na majeraha ameachwa mbali na mshindani wake lakini anafurahi mastaa wawili wa timu yake wanaongeza idadi ya kutupia na kuisaidia Simba.

“Kasi imekuwa kubwa mshindani wangu ameniacha mbali ni kutokana na mimi kukosa mechi nyingi kutokana na kukaa nje ya uwanja kwa muda Saido na Bocco wanafanya vizuri wamekuwa bora kwenye eneo la kufunga ndani ya timu hili linanipa furaha,” alisema na kuongeza;

“Wamebakiza bao moja kila mmoja kunifikia, sio mbaya kwani nacheza nao timu moja hivyo kukosekana kwangu inaonyesha hakuna kilichoharibika japo wananiongezea presha nikiwa nje ya uwanja inayonifanya nikipata wakati mzuiri wa kuitumikia timu natakiwa kujipanga.”

Alisema ubora wa safu ya ushambuliaji ya Simba kwa sasa ambayo imekuwa ikitupia kila mchezo inamuongezea presha akiwa nje ya uwanja kutokana na kuhofia namba yake ndani ya timu huku akiweka wazi kuwa anaendelea vizuri muda wowote atarudi kuongeza nguvu kikosini.

“Nimeanza mazoezi na wenzangu lakini bado nipo chini ya uangalizi wa daktari wa viungo.”