Pamba yajibu mapigo, yaifuata Coastal kwa ndege

Muktasari:

  • Pamba SC itarudiana na Coastal Union katika mchezo wa mtoano (playoff) ili kufuzu kucheza Ligi Kuu msimu ujao, mchezo ambao utapigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
  • Katibu Tawala Mkoa, MNEC wawajaza wachezaji morali

TImu ya Pamba SC ya jijini Mwanza imeondoka hii leo kwa usafiri wa ndege kuelekea jijini Tanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa mtoano (Playoff) dhidi ya wenyeji wake, Coastal Union ambao utapigwa Jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani jijini humo.

Timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza uliopigwa jana katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Kikosi cha wachezaji 25, viongozi sita wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa timu waliwasili katika uwanja wa ndege wa Mwanza saa10:30 asubuhi wakitarajiwa kuondoka saa 6:00 mchana kupitia uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) ambapo watachukua usafiri maalum wa gari kuwapeleka jijini Tanga.

Akiwaaga wachezaji hao uwanjani hapo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ngussa Samike amesema wamejiandaa kwa namna yoyote ili timu hiyo ipate ushindi ili kucheza Ligi Kuu kwani ni aibu kwa jiji hilo kukosa mwakilishi kwenye michuano hiyo mikubwa, huku akisistiza kuwa sapoti hiyo itaendelea kwa timu nyingine ikiwemo Toto Africans, Mbao FC na Alliance.

Bila kuweka wazi msaada walioutoa kwa timu hiyo, Samike amesema kuwa wamehakikisha kwamba wachezaji wamepata stahiki zao, maslahi, chakula na mazingira ya kufikia timu hiyo ni salama, ambapo amesema mkoa unayo matumaini makubwa kuwa wataibuka na ushindi.

Jamal Abdul, Mjumbe wa NEC mkoa wa Mwanza, amewaahidi wachezaji kuwa wadau wa timu hiyo wamejipanga kwa kila hali kuhakikisha kwamba motisha kubwa zitatolewa endapo wataibuka na ushindi ugenini dhidi ya Coastal Union.

"Nawaomba sana twendeni tulete ushindi, nawaahidi mtafurahi, hatukuja kwa siasa tunawahakikishia mtafurahi, sisi na wadau wote tumejiandaa kuhakikisha mnafanikiwa," alisema Abdul.