Pacome, Aucho wapewa kazi maalum

Muktasari:

  • Lakini kocha wa mabingwa hao wa Tanzania Miguel Gamondi ametamka kwamba kuna uwezekano mkubwa Pacome Zouzoua na Khalid Aucho wakafanya kazi kubwa kwenye mechi ya Ijumaa.   

JANA saa 7:30 mchana msafara wa kikosi cha Yanga ulikanyaga ardhi ya Afrika Kusini ukiwafuata wapinzani wao Mamelodi Sundowns.

                   
Lakini kocha wa mabingwa hao wa Tanzania Miguel Gamondi ametamka kwamba kuna uwezekano mkubwa Pacome Zouzoua na Khalid Aucho wakafanya kazi kubwa kwenye mechi ya Ijumaa.        


Yanga itakiwasha na Mamelodi kwenye mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye Loftus Versfeld uliopo Jiji la Pretoria baada ya kutoka suluhu kwenye mechi ya awali.


Gamondi ameliambia Mwanaspoti kuwa Yanga iko tayari kwa mchezo dhidi ya Mamelodi na watawapa sapraizi nyingine baada ya baadhi ya mastaa wake afya zao kutengamaa haswa Aucho na Pacome.


Gamondi alithibitisha kikosi chake kitakuwa na mabadiliko baadhi baada ya viungo wake Aucho na Pacome kuanza mazoezi huku wasiwasi mdogo ukisalia kwa beki wake Yao Attohoula ingawa yuko nae Sauzi.


“Tumeondoka na kikosi kamili ambacho tunaona kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo tunawaheshimu Mamelodi lakini kitu kinachotuvutia ni kwamba familia yetu imekamilika sawasawa,”alisema Gamondi ambaye aliwapa kazi ngumu Mamelodi kwenye mchezo wa kwanza.


“Tunaweza kuwa na kikosi chenye mabadiliko ni sisi tutaamua tucheze vipi na tuanze na nani kwani wale waliocheza mechi iliyopita wako sawasawa lakini pia wale ambao walikuwa na shida ya afya baadhi wamekaa sawasawa.


“Aucho (Khalid) yuko kwenye nafasi kubwa ya kucheza kuliko wenzake naweza kusema asilimia themanini, Pacome naye amerejea anafuatia nyuma ya Aucho kuhusu Yao amekuja lakini tutaamua hukohuko cha kufanya,” alisema Gamondi ambaye Wasauzi hao wanamhofia kwani aliwahi kuwa Kocha wao na anawaelewa vizuri nje ndani.


Yanga inahitaji sare yoyote ya mabao au ushindi kwenye mchezo huo ili itinge nusu fainali ya mashindano hayo ikiwa ni rekodi kutokana haikuwahi kucheza hatua hiyo. Gamondi alisema kikosi chake kitanufaika na makosa itakayofanya Mamelodi ambayo imesheheni mastaa ghali.


Gamondi ambaye ni Muargentina alisema anajua kwamba Mamelodi ndio inayotakiwa hasa kutafuta ushindi ili ilinde hadhi yao ya kuwa Bingwa wa African Football League (AFL) ambapo makosa watakayoyafanya ndio yatakuwa mtaji kwa timu yake.


“Tunaiheshimu Mamelodi, kwetu sisi hatuna ambacho tumebakiza, nadhani mnakumbuka kwamba malengo yetu yalikuwa kufika robo fainali ambayo tupo sasa. Mamelodi ndio wenye kazi ya kuthibitisha mafanikio yao ya kuwa bingwa wa AFL,” alisema.


“Wanatakiwa kushambulia na kutafuta ushindi sisi tunajua tutapata vipi kile tunachokitaka kwenye mchezo huo, tutawaangalia wao wanacheza vipi dhidi yetu na sisi tufanye kipi, soka ni mchezo wa makosa tunataka kuyatumia makosa yao.

HOTELI YA USHINDI
Yanga imefikia hoteli ya nyota tano ya  The Capital ambayo kwa Mamelodi wana kumbukumbu nayo mbaya ambapo imewahi kutumiwa na Al Ahly na Petro Atletico ya Angola na zikapata matokeo chanya.  


Msimu wa 2021-22 Mamelodi ilikutana na Petro Atletico kwenye hatua kama hii ya robo fainali ambapo baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 nchini Angola, waliporejea uwanja wa Loftus Versfeld wakajikuta wanalazimishwa sare ya bao 1-1 na kutupwa nje ya mashindano Waangola hao wakitokea hoteli hiyo.

 
Jana usiku walipiga tizi kwenye uwanja uliopo karibu na wakarejea hotelini kufuatilia mechi ya ligi ya wenyeji wao.