Onyango kuwavaa Zambia

WAKATI mechi za kirafiki za kimataifa zilizo kwenye kalenda ya FIFA zinaendelea, leo Ijumaa saa 10 jioni kutakuwa na mtanange  kati ya timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' ambao wanawakaribisha Zambia.

Katika mechi hiyo, beki wa Simba, Joash Onyango ni miongoni mwa wachezaji wa Harambee Stars wanaotarajiwa kucheza mchezo huo.

Upande wa Zambia wao watawakosa nyota wao wawili Lary Bwalya na Cloatus Chama wote wanaichezea Simba ambapo waliondolewa kikosini kwa sababu ya kuchelewa kuripoti kambini.

Mchezo mwingine utakua kati ya Nigeria na Algeria ambapo kwenye michezo saba iliyopita ikizikutanisha timu hizi, Nigeria imeshinda mechi tano, Algeria wakishinda moja na kutoa sare mara moja.

Mechi nyingine ya kusisimua itazikutanisha Ghana ambayo ina mchezaji Yakub Mohamed anayeichezea Azam FC itacheza dhidi ya Mali.

Yakub ataungana na nyota wengine kama Adrew Ayew na Thomas Partey wa Arsenal kuwavaa Mali ugenini.

Timu ya taifa ya Cameroon wao wamesafiri mpaka Japan kucheza na timu ya taifa hilo, vita kubwa itakua kati ya mshambuliaji wa Liverpool, Takumi Minamino na kipa wa Ajax, Andre Onana.

Senagal yenye nyota kama Sadio Mane, Koulibaly na Kipre Diatta itakuwa ugenini kukipiga dhidi ya Morocco anayoichezea nyota mpya wa Chelsea, Hakim Ziyech.

DR Congo ya wakina Jackson Muleka nao pia wataingia uwanjani leo kucheza dhidi ya Burkina Faso ya nyota mpya wa Aston Villa Bertrand Traoré.

Michezo mingine itakuwa kati ya Togo na Libya, Tunisia na Sudan huku Mauritania watacheza dhidi ya Sierra Leone.

Mchezo wa mapema leo utakuwa kati ya Japan na Cameroon utakaopigwa saa 9 alasiri kisha mingine itafuata na mechi ya mwisho itakua kati ya Morocco na Senagal mchezo huo utachezwa saa 3 usiku.