Nyota wapya Stars kuivaa Uganda

Timu ya taifa 'Taifa Stars' mambo yameiva kuelekea mechi ya kirafiki ya kuadhimisha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika dhidi ya Uganda Cranes utakaochezwa Alhamisi katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
Meneja wa timu hiyo Nadir Haroub Cannavaro amesema kuwa wachezaji wote wamewasili kambini na amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi siku ya mchezo ili kuipa sapoti.
"Wachezaji wote wako kwenye hali nzuri na wameahidi kupambana kwa ajili ya timu yao," amesema.
Cannavaro aliongeza kuwa sababu ya kuitwa wachezaji wapya kwenye kikosi hicho ni kwa ajili ya kuijenga timu bora ya Taifa ya baadae.
"Wengi wamehoji sana baada ya kikosi kuitwa lakini niwatoe hofu Taifa letu limebarikiwa vipaji vingi hivyo ni nafasi kwao kuonyesha hilo," amesema.
Wachezaji 23, walioitwa kwenye mchezo huo ni Haroun Mandanda (Mbeya City), Musa Mbisa, Hans Masoud, Abdul Suleiman 'Sopu' (Coastal Union), Nathaniel Chilambo, Rashid Juma (Ruvu Shooting)
Kelvin Kijiri, Nickson Kibabage, Abdulrazack Mohamed (KMC), Oscar Masai, Kelvin Nashon (Geita Gold), Sospeter Bajana, Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Abdulmajid Mangalo, Denis Nkane (Biashara United)
Metacha Mnata, Tariq Simba, Vitalis Mayanga (Polisi Tanzania), Hassan Nossoro, Anuary Jabir, Cleophance Mkandala (Dodoma Jiji), Meshack Abraham (Kagera Sugar) na Reliant Lusajo wa Namungo FC.